Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili(MNH) imesema imefanikiwa kuzindua mtambo unaotumia tiba hewa yenye mgandamizo ya oksijeni kwa 100% (Hyperbaric Oxygen Therapy) ambao unatibu magonjwa zaidi ya 10.
Ambapo Tanzania inakuwa nchi ya kwanza katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, na ya pili Kusini mwa Jangwa la Sahara kupitia hospitali za umma kutumia mtambo huo uliogharimu mil.250 .
Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Machi 6,2025 na Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Hospitali ya Muhimbili,Upanga na Mloganzila,Dkt.Rechal Mhaville wakati akizungumza kuhusu mafanikio na utekelezaji wa hospitali hiyo katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo Prof.Mohamed Janab.
Dkt.Mhaville amesema kuwa hadi sasa wagonjwa 54 wamenufaika na huduma hiyo na kupona magonjwa mbalimbali ikiwemo vidonda sugu, maumivu makali ya mgongo na wagonjwa waliopata madhara ya mionzi tiba ya saratani.
Aidha Dkt.Mhaville amesema hospitali hiyo iliendelea kutoa huduma ya upandikizaji vifaa vya kusaidia kusikia ambapo watoto 54 walihudumiwa na kufanya idadi ya walionufaika kufikia 88 tangu kuanzishwa huduma hiyo nchini Juni 2017.Â
Amesema Serikali imewagharamia watoto hao 54 kila mmoja mil.45 sawa na bil. 2.43 ambapo kama wangeenda nje ya nchi Serikali ingelipa Mil. 120 Mil kwa kila mtoto sawa na bil. 6.5.
“Kutokana na hilo Serikali imefanikiwa kuokoa kiasi cha bil. 4 na Tanzania ni nchi ya kwanza kutoa huduma hii kupitia hospitali za umma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki,”amesema.Â
Vilevile Dkt.Mhaville amesema Katika kipindi cha miaka minne iliyopita,hospitali imefanikiwa kuanzisha huduma ya ubingwa bobezi wa kupima watoto wachanga kiwango cha kusikia mara tu wanapozaliwa ili kugundua mapema na kutoa matibabu.Â
Ambapo amesema tangu kuanzishwa huduma hiyo mwishoni mwa 2023 tayari watoto wachanga 320 wamenufaika ambapo waliokutwa na changamoto hizo wako kwenye mpango maalum wa ufuatiliaji ikiwemo mafunzo ya kuongea na baadaye kupandikizwa vifaa vya kuwasaidia kusikia.
Aidha amesema hospitali hiyo imeanzisha huduma za kuweka magoti na nyonga bandia Katika kampasi ya Mloganzila wagonjwa waliopata maradhi ya viungo vya magoti 207 na nyonga 59 waliweza kupata huduma mpya zilizoanzishwa katika kampasi ya Mloganzila na wagonjwa 10 walifanikiwa kufanyiwa upasuaji wa marejeo wa magoti na nyonga bandia.
Pamoja na hayo amesema hospitali hiyo imefanya upasuaji rekebishi wa kutengeneza Taya jipya kutumia Mifupa iliyovunwa kwenye mbavu na mfupa wa nyonga.Â
“Tulianzisha huduma ya kuondoa sehemu yenye ugonjwa kwenye taya kisha kuvuna sehemu ya mbavu pamoja na mfupa wa nyonga kwa kutumia vipandikizi maalum kuunda mfupa wa taya jipya la chini ili kumrejeshea mgonjwa muonekano mzuri lakini pia huweza kupandikizwa meno na kumrejeshea mgonjwa uwezo wa kula tena.
“Pia tumeanzisha matibabu ya kuziba mapengo ambapo mzizi bandia hupandikizwa kwenye taya, kisha kuwekewa meno juu yake yanayogandishwa na kutumika kama sehemu ya meno yake ya kuzaliwa nayo,”amesema.
Dkt.Mhaville ameeleza kuwa serikali imewezesha hospitali hiyo kununua mashine ya kisasa kabisa inayowezesha uchunguzi wa magonjwa ya mifupa ya taya pamoja na CT scan ya uso na kichwa kusaidia kupanga upandikizaji wa vipandikizi vya meno ambapo tangu kununuliwa mwishoni mwa mwaka 2024 tayari wagonjwa 2,251 wamenufaika.
“Hospitali imefanikiwa pia kuanzisha huduma ya matibabu ya mzio nchini na yenye watalaam wabobezi wa kutoa huduma za upimaji na matibabu ya mzio (allergy). Jumla ya wananchi 470 wametibiwa tangu kuanzishwa kwa huduma hii mwaka jana 2023 ambapo MNH ni hospitali ya kwanza kutoa huduma hii kwa kiwango cha ubobezi hapa nchini.
Pamoja na huduma mionzi tiba kwa wagonjwa wa ngozi ambapo hospitali imefanikiwa kuanzisha matibabu ya magonjwa ya ngozi kwa njia ya tiba mwanga (phototherapy) na tiba laser ikiwa ni hospitali pekee nchini inayotoa huduma hii. Huduma hii imekuwa msaada mkubwa kwa wagonjwa wenye matatizo ya vitiligo na saratani za ngozi ambapo wastani wa wagonjwa 10 hadi 15 wanahudumiwa kwa wiki. (tatooo)

More Stories
BUWSSA yapokea bil.28.1 ya miradi,serikali awamu ya sita
STANBIC yaendelea kusaidia makampuni madogo ya uchimbaji mafuta na gesi
Mawakala kielelezo cha uwazi uboreshaji daftari la wapiga kura