September 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mtumushi TRA apandishwa kizimbani tuhuma za Rushwa

Na Jumbe Ismailly, TimesMajira Online, Nzenga

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Nzega, Mkoani Tabora imempandisha kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Wilayani hapo mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dickson Mtandu Mtandu (52) kwa tuhuma za kuomba rushwa ya shilingi milioni 1.5 kutoka kwa mfanyabiashara wa nyumba ya kulala wageni.

Mwendesha Mashitaka wa TAKUKURU Wilaya ya Nzega, Mazengo Joseph amedai, mtumishi huyo wa TRA alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) (2) na 3(a) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa Na.11/2007.

Awali Mwendesha Mashtaka huyo alidai mbele ya Hakimu wa Wilaya ya Nzega, Joseph Mwita kuwa, kati ya Agosti 26 na 28 mwaka huu, kwa nyakati tofauti mshitakiwa akiwa eneo la Mery Pud mjini Nzega, aliomba rushwa ya shilingi milioni 1,500,000/= kutoka kwa Sahani Katuli ili asimchukulie hatua za kisheria kwa kutotoa risiti ya EFD katika nyumba yake ya kulala wageni ya Kipozo ilioko mjini Nzega.

Pia Agosti 29 mshitakiwa alikamatwa na Maafisa wa TAKUKURU Wilaya ya Nzega wakati akipokea rushwa ya shilingi laki nne kati ya shilingi 1,500,000/= alizokuwa ameomba kutoka kwa mlalamikaji ambaye ni mfanyabiashara wa nyumba ya kulala wageni baada ya kuwekewa mtego na taasisi hiyo.

Hata hivyo, mshitakiwa huyo baada ya kusomewa shitaka, alikana kutenda kosa hilo ambapo mshitakiwa huyo yupo nje kwa dhamana ya shilingi milioni moja na wadhamini wawili hadi Oktoba 20 mwaka huu itakapotajwa tena.