January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mtoto wa mwaka mmoja na miezi kumi,adaiwa kubakwa na baba wa kambo

Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Mwanza

Doto Maduhu(32),fundi ujenzi na mkazi wa Kishiri wilayani Nyamagana mkoani Mwanza,anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumbaka,kumlawiti na kumshambulia mtoto wake wa kambo,mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi kumi,jina limehifadhiwa ambaye alifariki katika harakati za kupatiwa matibabu.

Pia mama mzazi wa mtoto huyo aitwaye Aneth Mhano(23), mkazi wa Kishiri,anashikiliwa kwa kushindwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi au majirani ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Akizungumza Januari 6,2024,na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa, amesema mnamo Desemba 30,2024, majira ya saa 4 usiku (22:00hrs),jeshi hilo lilipata taarifa kuwa mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi kumi ambaye jina lake wanalihifadhi kwa mujibu wa sheria, kuwa amefanyiwa ukatili na baba yake wa kambo aitwaye Doto Maduhu Sita,huku chanzo cha tukio hilo likidaiwa ni tamaa ya ngono.

Mutafungwa amedai kuwa,mtoto huyo alikuwa anafanyiwa ukatili huo mara kwa mara, na kusababisha hali yake ya kiafya kuwa dhaifu na kuwafanya raia wema kutoa taarifa kwa Jeshi la polisi kupitia dawati la jinsia na watoto.

“Baada ya kupata taarifa hizo, jeshi la polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto,tulifanya ufuatiliaji wa haraka kupitia taarifa hiyo na kufanikiwa kumkamata Doto, kwa tuhuma za kumbaka, kumlawiti na kumshambulia mwanaye huyo wa kambo,”amesema Mutafungwa.

Kutokana na taarifa hizo polisi walifika eneo la tukio na kumkuta mtuhumiwa huyo akishirikiana na mke wake aitwaye Aneth(mama mzazi wa mtoto huyo),wakiwa katika jitihada za
kumpeleka mtoto huyo ili apate tiba.

Ambapo walifika kituo cha afya cha Usumau kilichopo Kishiri na walielekezwa kumpeleka mtoto huyo katika zahanati ya Serikali Igoma. Katika harakati za matibabu mtoto huyo alifariki dunia Desemba 30,2024
majira ya saa 4 usiku (22:00hrs) katika zahanati hiyo ya Igoma.

“Pamoja na kumkamata mwanaume huyo pia tunamshikilia na kuendelea kumhoji mama
mzazi wa mtoto huyo, kwa kushindwa kutoa taarifa kwa polisi au kwa jirani zake,juu ya ukatili aliokuwa akifanyiwa mtoto ili hatua za
kisheria ziweze kuchukuliwa na kuokoa maisha ya mtoto huyo,”.

Hata hivyo Mutafungwa,amesema mwili wa mtoto huyo umefanyiwa uchunguzi na madaktari na umekabidhiwa kwa baba mzazi wa mtoto huyo aitwaye Emmanuel Daud(28), dereva na mkazi wa Maduka Tisa, Wilaya ya
Ilemela na ndugu wengine kwa ajili ya mazishi.

“Uchunguzi kuhusiana na tukio hili
unaendelea na hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kuhusika
katika ukatili huo ambao umesababisha kifo,”amesema.

Sanjari na hayo, Mutafungwa,ametoa wito kwa wananchi hususani wazazi na walezi
kuchukuwa tahadhari na kuzingatia malezi bora ya watoto, ili kuwaepusha na vitendo vya
ukatili.

“Tunawakumbusha kuwa vitendo vya ukatili kwa watoto hufanywa na watu walio
karibu na watoto, kwa misingi ya undugu, malezi na ujirani aidha, tunawakumbusha
kuendelea kutembelea madawati ya jinsia na watoto yaliyopo kwenye vituo vyetu vya
polisi kwa kutoa taaarifa kuhusu matukio yote ya ukatili wa kijinsia,”. amesema Mutafungwa.