Na Moses Ng’wat, TimesMajira Online, Songwe.
SERIKALI kupitia Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba, imefanya uamuzi kwa kusema kuwa itautumia mto momba kama chanzo katika mradi wa kusambaza maji kwenye miji ya Tunduma , vwawa na mlowo badala ya chanzo kilichopendekezwa awali cha mto bupigu uliopo wilayani ileje.
Uamuzi huo umetangazwa ikiwa ni siku chache tuu baada ya Waziri wa Maji,Juma Aweso, kufika na kumuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kufika Mkoani hapa ili kumaliza mvutano uliojitokeza juu chanzo kipi cha maji kati ya mto Bupigu na Momba unaweza kuwa ni suluhisho la kudumu la usambaza maji ya uhakika katika miji hiyo.
Katika kikao cha mwisho cha Kamati ya ushauri (RCC) ya Mkoa wa Songwe kuliibuka mvutano mkali ambapo baadhi ya wajumbe wakiongozwa na Naibu Waziri walitaka maji ya Mto Bupigu ndio yatumike kama chanzo cha mradi wa kusambaza maji katika mji wa Tunduma, huku baadhi ya wajumbe wakitaka mto Momba ndio utumike kwa kuwa maji yake ni ya uhakika kwa mwaka mzima.
Katibu Mkuu, Mhandisi Kemikimba baada ya kuwasili jana Mkoani hapa kwa ziara ya siku moja alimwambia Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Francis Michael kuwa uamuzi uliofikiwa na wataalam baada ya kazi za usanifu kufanyika katika mito hiyo miwili, mto Momba ndio wenye maji ya uhakikana kutosha kwa ajili ya mradi huo.
Alisema wameamua kutumia mto Momba kwa sababu kwenye sanifu za awali ilikuwa watumie mto Bupigu wa Ileje lakini baada kukusanya takwimu mto Bupigu kiangazi maji yake yanapungua tukaona sio sahihi kuweka mradi wa chanzo cha maji wa kubeba Lita milioni 70 alafu maji kiangazi maji yanapungua tukaona sio sahihi.
” Sanifu zineoneaha kuwa mto Momba una maji ya kutosha hata tukichukua lita milioni 70 bado maji yataendelea kutililika na ndio chanzo sahihi kuhudumia mji wa Tunduma ambao umekuwa na changamoto kubwa ya Maji kwa muda mrefu” alisisitiza Mhandisi Kemikimba
“Mji wa Tunduma tu unahitaji Lita milioni 23 za maji kwa siku sasa visima haviwezi kutosheleza ndio sababu wizara ya Maji tunahitaji kutumia vyanzo vya uhakika kutatua changamoto ya maji”. aliongeza Mhandisi Kemikimba
Alisema katika mradi huo ambapo awali utaanza kutekelezwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 70, kutajengwa matangi ya maji yenye uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo milioni 5 hadi milioni 10 ili kusambaza kwa wananchi wa miji hiyo.
Katika hatua nyingine Mhandisi Kemikimba alisema itaendelea na kuwaondoa wakandasi wote ambao hawawezi kuendana na kasi ya Wizara ya Maji na kwamba mchakato wa kuvunja mkataba na mkandarasi HELPDESK anyetekeleza mradi wa maji wa Itumba -Isongole wenye gharama ya shilingi bilioni 4 unaendelea vizuri.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Michael alisema mradi huo wa maji wa bilioni 70 utaanza kutekeleza kwa miezi 24 .
Dkt. Michael alisema Mkoa huo bado una tatizo la upatikanaji maji katika mji wa Tunduma, Mlowo na Vwawa ambapo kwa sasa hali ya upatikana wa maji ni asilimia 48, katika miji ya Tunduma wakati vijijini upatikanaji ni asilimia 78 .
More Stories
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango