December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MTIMA: Sare za  mei mosi zilifata taratibu zote za manunuzi

Na Penina Malundo.timesmajira,Online

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU),Rashid Mtima amesema sare za mei mosi za mwaka 2022 zilizingatia taratibu zote za manunuzi kwa mujibu wa kanuni za manunuzi ya Chama za mwaka 2018 na kitabu cha zabuni namba TALG/PROC/0021/2021.

Pia amesema mchakato wa kumpata mzabuni wa sare hizo ulifata utaratibu wote na kumpata mzabuni Savana General Merchandise ambaye alipewa kazi ya uchapaji na usambazaji wa sare 80,000 zenye thamani ya Bilioni 1.1.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam,Mtima amesema baada ya mapokezi ya sare hizo ikagundulika kwamba kuna mapungufu makubwa ya ubora wa sare ikilinganishwa na makubaliano waliyokubaliana kwa mujibu wa mkataba.

“Ofisi yetu ilichukua maamuzi ya kumjulisha mzabuni huyo kuhusu mapungufu hayo na kumtaka kusimamisha zoezi la usambazaji sambamba na kuwajulisha Makatibu wa Mikoa ambayo ilishapokea kutozigawa sare hizo kwa wanachama kwa sababu ya mapungufu makubwa yaliyogundulika,”amesema na kuongeza

“Taratibu za ndani kwa kuzingatia kitabu cha zabuni,kanuni za manunuzi ya chama toleo la mwaka 2018 na mkataba zinaendelea hadi sasa tumekutana na mzabuni na kufanya nae mazungumzo ikiwemo kurudisha fedha kulingana mkataba unavyosema na akigoma hatua za kisheria zinachukuliwa ,”amesema Mtima

Aidha Mtima amesema sio kweli kama kikundi cha watu wenye nia ovu ya kuchafua chama kilivyosema kuwa kiasi cha Sh.Bilioni 1.1 za kuchapwa sare 80,000 zilipigwa kwa kumlipa mzabuni, bali mpaka sasa mzabuni amelipwaa kiasi cha sh.Milioni 700 kwa mujibu wa mkataba.

Mtima amesema TALGWU ina taratibu zake za kumtafuta  Mzabuni kwa mujibu wa kanuni za manunuzi za Chama toleo la 2018 kwa ajili ya zabuni zote ambazo kampuni au wazabuni huomba kwa kila mwaka na si kuletwa na kiongozi au mjumbe wa bodi ya zabuni kama ilibvyopotoshwa na baadhi ya watu.

 Akizungumzia Sare za mei mosi za mwaka 2020
Mtima amesema  ununuzi wa sara za sherehe za mei mosi mwaka huo 2020,uligharimu kiasi cha sh. Bilioni 1.1 na sio Bilioni 1.2 kama ilivyopotoshwa na kikundi cha watu wachache wasiojua ukweli wowote.

“Idadi ya sare zilizochapishwa kwaajili ya mei mosi kwa wanachama wake wote na haijawahi kutokea mwanachama akakosa au kujinunulia sare ya mei mosi yeye mwenyewe,huu ni upotoshaji unaofanywa na vikundi vya watu wachache waliowahi kufanya kazi katika Chama hiki kuongea uongo ili kuona chama kinavurugika jambo ambalo sio kwetu,”amesema na kuongeza

“Huu ni upotoshaji na uongo uliokithiri wenye dhamira ovu ya kuichafua TALGWU na uongozi wake kwani ukweli ni kwamba ununuzi wa sare za mei mosi mwaka 2019 uligharimu kiasi cha sh.Milioni 935 kwa idadi ya fulana 80,000 na kofia 80,000 na haijawahi kutokea ofisi za mikoa zikakosa kofia na kujinunulia,”amesema

Akizungumzia suala la ununuzi wa magari ya Ofisi hiyo.

Mtima amesema manunuzi yote ya magari yanazingatia kanuni za manunuzi ya Chama toleo la mwaka 2018 pamoja na Bajeti ya Chama inayopitishwa na Baraza Kuu la Chama Taifa hivyo ununuzi wa gari ulizingatia taratibu zote za chama kuanzia mchakato wa ununuzi,bajeti ya Chama na hali ya kifedha.

Amesema Chama chao hakikuwahi kuthamiria kununua gari jipya kwa kuwa uwezo wa kutenga Milioni 400 kwaajili ya gari la Katibu hawana.”Hivyo chama kilitenga kununua fedha za gari ya mtumba aina ya Toyota Land Cruiser V8 na gari hilo halikuwahi kuwa na kadi mbili kama baadhi ya watu wenye nia ovu wanavyosema,”amesema

Ameendelea kusema kila mwaka chama chao kinatangaza zabuni mbalimbali ikiwemo matengenezo ya magari na kwa kipindi cha mwaka 2015 kampuni ya Bamba Auto Works ilikuwa na mkataba na chama wa kutengeneza magari ya TALGWU na taratibu zote zilizingatiwa.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za mitaa Tanzania (TALGWU) , Bw.Rashid Mtima akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi  wa habari leo mei 26,2022 katika Ofisi za Chama hicho Jijini Dar es Salaam