Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online Morogoro
BAADA ya kufanikiwa kusalia kwenye michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) msimu ujao, timu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro imewaangukia mashabiki wake na kuwaomba radhi kwa kutokuwa na msimu mzuri.
Mtibwa imefanikiwa kusalia katika Ligi hiyo baada ya ushindi wa goli 2-1 walioupata kwenye uwanja wa CCM Gairo dhidi ya maafande wa Ruvu Shooting.
Ushindi huo umewafanya Mtibwa ambao walishinda mechi 11, sare 12 na kupoteza mechi 15 kumaliza msimu huu wakiwa nafasi ya 14 na pointi zao 45 tofauti na msimu uliopita ambao walimaliza Ligi wakiwa nafasi ya tano baada ya kushinda mechi 14, sare nane lakini wakipoteza mechi 16.
Afisa habari wa timu hiyo, Thobias Kifaru ameuambia Mtandao huu kuwa, anawashukuru wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kwa maombi yao huku akiwaomba radhi kwa timu yao kutokuwa na msimu mzuri jambo lililowaweka kwenye hatari ya kushuka daraja.
Amesema, katika kipindi ambacho timu yao ilikuwa kwenye wakati mgumu wa kupambania kutoshuka daraja, mashabiki wao waliendelea kuwa nao bega kwa bega katika maombi na Mungu aliyasikia.
Kifaru amesema kuwa, baada ya jambo hilo kupita, sasa wanarudi upya kujipanga kwa ajili ya msimu ujao ambao watahakikisha hawapitii kwenye kipindi na wakati mgumu kama waliokuwa nao msimu huu.
Amesema, kasoro zote ambazo zimewayumbisha wanarudi kuzifanyia kazi ili kuifanya timu hiyo kuwa bora, kufanya vizuri na kurudi kwenye makali yao katika msimu huo mpya.
“Tuna kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha tunaondoa karoro zote zilizotuangusha msimu huu na kurudi kwenye ubora wetu katika msimu ujao kwani tunaamini tuna kazi kubwa ya kujenga kikosi bora lakini na kuwapa zawadi mashabiki wetu ambao walikuwa na huzuni kubwa,” amesema Kifaru.
More Stories
Watumishi wa Fahari wafanya Bonanza
Rais Samia atia mkono mchezo wa masumbwi Tanzania
Chino bingwa mpya wa IBA Intercontinental Championship