January 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mtega: Tutajenga malambo, kutenga maeneo ya malisho

Na Esther Macha, TimesMajira Online, Mbarali

MGOMBEA ubunge Jimbo la Mbarali kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Francis Mtega amesema endapo atapewa ridhaa na wananchi wa Wilaya hiyo atahakikisha anashirikiana na Serikali kujenga malambo ya kunyweshea mifugo na kutenga maeneo ya malisho.

Mtega ameyasema hayo wakati wa mkutano wa kampeni wa kunadi sera za chama hicho kwa wananchi wa kata ya Mapogoro

Alisema, akipewa ridhaa ya kuwa mbunge, atahakikisha changamoto ya watumishi idara ya kilimo na mifugo inapatiwa ufumbuzi ikiwemo kusimamia madawa ya mifugo ili yaweze kufika kwa wakati kwa wafugaji.

Kuhusu elimu Mtega alisema kuwa, endapo akichaguliwa ataongeza motisha kwa walimu wa shule za msingi na sekondari kwa kuwapa fedha ili waweze kuongeza ufanisi zaidi wa kuwafundisha watoto.

“Hivi sasa Mkoa wa Mbeya unafanya vizuri kielimu kwani awali tulikuwa na ufaulu wa asilimia 67 na mpaka sasa Mkoa umefikisha asilimia 85 hivyo tuna kila sababu ya kuwapa motisha walimu kwa kutambua mchango wao mkubwa katika sekta ya walimu,” alisema Mtega.

Kwa upande wake Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Mbarali, Kassim Kondo amewataka wananchi kuacha ushabiki kwa vyama visivyokuwa na ilani badala yake wachague CCM ambayo itawaletea maendeleo ya kweli.

Mgombea udiwani viti maalum kata ya Madibira, Paskalina Ngungulu amesema, atashirikiana na Mbunge katika kutatua changamoto za wananchi ikiwemo kero ya Maji, Zahanati pamoja barabara .