January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mtaturu apendekeza njia bora za kilimo

Na Doreen Aloyce, Dodoma

MBUNGE wa Jimbo la Singida Kaskazini, Miraji Mtaturu amesema ili kilimo kiwe chenye tija hapa nchini Serikali inapaswa kuweka nguvu katika utafiti wa mbegu bora zitakazosaidia kuzalisha mazao ya kutosha badala ya kulima eneo kubwa bila mafanikio.

Kauli hiyo ameitoa bungeni Dodoma wakati alipokuwa akichangia bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2021/22 jinsi gani sekta ya kilimo inavyopaswa kunufaisha jamii kwa ujumla.

Miraji amesema kuwa, juhudi zinatakiwa kuongezwa kwenye kilimo kwani kimebeba uchumi wa nchi ambapo kwa asilimia 80 ya wananchi wanajihusisha na kilimo,wanapata mahitaji mbalimbali ikiwemo kusomesha watoto.

Amesema kuwa,kuna haja ya Serikali kutoa ruzuku na kuangalia mbegu zenye tija ambazo zitabadilisha kilimo kwa watanzania ambazo mbegu hizo zitakuwa na uwezo wa kulima eneo dogo, lakini uvunaji unakuwa mkubwa.

‘’Niishauri Serikali yetu kwenye upande wa mbegu hatuwezi kubadilisha kilimo chetu kama hatutaweka utafiti zaidi kwenye mbegu, wananchi wataweka nguvu, lakini hatutasonga mbele wenzetu wa nchi zingine wanalima eneo dogo lakini wanapata uzalishaji mkubwa kutokana na utafiti mkubwa walioufanya kwenye mbegu,’’amesema Mtaturu.

Aidha, amesema anasikitika kuona Serikali inatumia fedha nyingi kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi ili hali kuna ardhi ya kutosha na kuna mazao ambayo yanaweza kuzalisha mafuta hayo ambayo yanaweza kuuzwa huko nje.

‘’Nitajikita kwenye zao la alizeti kwa hapa Tanzania tuna ardhi kubwa ya kutosha ambayo tungelima na kupata mafuta ya kutosha, lakini cha kushangaza hapa Tanzania tunaagiza nje ya nchi na kila mtu analia na bei ya kupanda kwa mafuta hizo fedha bora zingetumika kufanya utafiti,”amesema.

Pia amesema, kilimo cha umwagiliaji kipewe nafasi kubwa kwa kuongezewa wataalamu kwenye halmashauri mbalimbali hapa nchini ambao watasaidia kuongeza uzalishaji mkubwa na sio kuwaachia wakulima tu ambao hawana utaalamu na hatimaye fedha zinaharibika na tutapata uzalishaji mkubwa kuvuna maji ya mvua.

‘’Tukiwa makini kwenye kilimo tutasonga mbele nisisitize suala la masoko ya uhakika ili wakulima wakivuna wajue wapi wanaenda kuuza jambo ambalo hili litaondoa mkulima kuuzia kwenye mashamba kabla hajavuna,’amesema.

Hata hivyo aliitaka Serikali kuangalia suala la mikopo kwa Benki ya kilimo ambayo imekuwa na masharti ambayo sio rafiki kwa wakulima walioko vijijini kwamba katika Jimbo lake eneo la Igungi kuan Amkosi walikopeshwa million 85 msimu uliopita hapakuwa na mvua za kutosha wakapelekwa mahakamani jambo ambalo linapoteza matumaini kwa wakulima kutumia Benki hiyo.

‘’Hizi Benki za kilimo ziwe Rafiki na msaada kwa wakulima kuwawezesha kuwapatia pembejeo na sio kuwaangamiza utakuta wana makubaliano na mikataba lakini mwisho wa siku msimu unapokuwa mbaya wanaanza kuburuzwa mahakamai hali hiyo hawewezi kurudi kukopa kwani haimasaidii mkulima bali kumnyonya,”ameongeza Mtaturu.