Na Mwandishi Wetu, Tunduru
MKUU wa wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro ameahidi kuboresha maslahi ya wachezaji, benchi la ufundi pamoja na timu mzima ya Tunduru Korosho ambao wamefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Mikoa.
Mbali na ahadi hiyo pia amewataka wachezaji wa timu hiyo kutobweteka na mafanikio waliyoyapata, badala yake waongeze bidii ya mazoezi ili wafanye vizuri katika mashindano ya Ligi Daraja la Pili Taifa (SDL).
Mtatiro ametoa kauli hiyo wakati wa mapokezi ya timu hiyo katika viwanja vya Baraza la Idd Mjini Tunduru yaliyohudhuriwa na mamia ya wakazi wa mji huu mara baada ya timu hiyo kuwasili ikitokea Kigoma katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa.
Mtatiro ambaye pia ni mlezi wa Tunduru Korosho amesema, baada ya kutwaa ubingwa wa mabingwa wa Ligi ya mabingwa wa Mikoa, timu hiyo inahitaji maandalizi ya uhakika sana ili kujiweka fiti kwa ushiriki wa ligi daraja la pili Taifa ambapo itakutana na timu nyingine zenye uwezo mkubwa.
Mlezi huyo amesema, fedha ambazo watalipwa wachezaji na benchi la ufundi zitakazotokana na michango ya wananchi wa Tunduru hususani kutokana na fedha za korosho ambazo kila mwananchi atalazimika kuchangia.
Sambamba na hilo Mtatiro amewataka wananchi kufahamu kuwa timu hiyo ni wananchi wote wa Tunduru, hivyo wanapaswa kuiunga mkono kwa kuchangia fedha ili iweze kujiendesha na kufanya vizuri katika mashindano yajayo ya Ligi daraja la pili Taifa.
Katika hatua nyingine mkuu wa Wilaya amesema, kwa kushirikiana na Chama cha Mapinduzi watahakikisha wanaufanyia ukarabati mkubwa Uwanja wa michezo wa CCM Wilaya unaotumika kwa ajili ya michezo mbalimbali ya mpira wa miguu ili uwe bora na utumike kwa ajili ya ligi inayokuja.
Ukarabati wa uwanja huo utafanyika kabla ya kuanza kwa Ligi Daraja la pili ambapo Timu ya Tunduru Korosho itashiriki baada ya kuibuka mabingwa wa, Ligi ya Mabingwa Taifa mashindano yaliyozishirikisha Timu 8 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa timu ya Tunduru Korosho, Mohamed Kiyonjo amewashukuru wakazi wa mji huo kwa kujitokeza kwa wingi kuipokea timu hiyo na kusema kuwa hali hiyo imeleta hamasa kwa wachezaji wa timu hiyo kufanya vizuri zaidi katika mashindano yajayo.
Kiyonjo amesema, ni faraja kubwa kuona idadi kubwa ya wananchi wamejitokeza kuipongeza na kuipokea timu yao ambapo ametumia nafasi hiyo kuwaomba wana Tunduru kuendelea kuiunga mkono Timu ili iweze kufanya vizuri zaidi katika michezo yake.
Hata hivyo amekiomba Chama cha Mapinduzi kuharakakisha kuufanyia ukarabati uwanja wa michezo wa CCM ambao utatumika kama uwanja wa nyumbani kwa timu hiyo.
More Stories
Watumishi wa Fahari wafanya Bonanza
Rais Samia atia mkono mchezo wa masumbwi Tanzania
Chino bingwa mpya wa IBA Intercontinental Championship