January 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mtango kumrudisha Mwazoa ulingoni

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

BINGWA wa Dunia wa mkanda wa UBO uzito Light Weight Mtanzania Salim Mtango yupo mbioni kumrudisha katika tasnia ya ngumi za kulipwa promota wa mchezo huo mwenye maskani yake jijini Tanga, Ally Mwazoa aliyetangaza rasmi kujiweka pembeni wiki iliyopita.

Kupitia sauti aliyoituma kwa wadau mbalimbali ikiwemo mabondia, Mwazoa alisema, ameamua kusitisha shughuli zote za kudhamini mapambano ya ngumi baada ya kudiziwa na majukumu yake binafsi na kuona kwakuwa amekaa zaidi ya miaka 20 akidhamini na akilea vijana katika mchezo huo hivyo sasa ni muda muafaka kwake kujitoa.

Licha ya maamuzi yake ya kujitoa lakini aliwaomba wakazi wa Tanga wenye uwezo kujitoa na kuendelea kukuza vipaji vya vijana hao ili Tanga iendelee kung’ara katika mchezo huo huku pia akiwaomba mapromota aliokuwa akishirikiana nao wasiwaache mabondia wa Tanga bila kuwashirikisha katika mapambano yao kwani kila mmoja anakiri Tanga ina vipaji vikubwa ambavyo vikilelewa vitaweza kuwakilisha Taifa hili katika mapambano makubwa duniani na kufanya Tanzania izidi kutambulika kimataifa kupitia mchezo huo.

Lakini licha ya kutoa taarifa hiyo, mmoja wa watu wa karibu wa promota huyo ameuambia kuwa, kilichomfanya kocha huyo kuamua kujiondoa katika ngumi ni baadhi ya mambo yasiyo ya kweli yalianza kuzushwa juu yake.

Amesema kuwa, katika miaka yote ambayo promota huyo ameandaa mapambano hakuwahi kukutwa na kashfa ya kuzulumu bondia, hivyo ameona ajiweke pembeni kuepuka nia ovu dhidi yake.

“Katika mapambano matatu yaliyofanyika kabla ya kutangaza kujiweka pembeni yalikuwa ni kama yameingia fitna na ili kulinda heshima yake aliyoiweka kwa miaka karibu 20 ameamua kujiweka pembeni na kuwaachia wengine, “.

Kujiondoa kwa Mwazoa katika mchezo huo kulikuwa mwiba kwa mabondia wengi kutoka Tanga ambao asilimia kubwa wamekuzwa na kuibuliwa kupitia kambi hiyo akiwemo Mtango ambaye hakuamini adi pale alipozumngumza naye ana kwa ana.

Akizungumza na Majira Mtango amesema kuwa, baada ya kuzungumza kwa kina na promota huyo amesema, alichoamua ni kujitoa kwenye kuandaa mapambano na atabaki kuwa kama mshauri tu.

Majibu hayo yalikuwa ni tumaini jipya kwa Mtango ambaye amemuomba kuwa mshauri wake na kuahidi kuwa hatokata tamaa kuzungumza naye hadi pale atakapokubali kuwa Meneja wake.

“Kiukweli nilizungumza mambo mengi na promota Mwazoa na amekubali kusimama kama mshauri au kuwa meneja na si kuandaa mapambano hivyo kutokana na umuhimu wake kwangu nimemuomba awe amshauri wangu lakini bado nataka kumshawishi na kumuomba zaidi ili asimame kama meneja wangu na najua hatokataa, ” amesema bingwa hiyo.

Hata hivyo amesema kuwa kwa sasa yupo katika maandalizi ya pambano lake la Novemba 28 dhidi ya bondia kutoka nchini Ghana anayefanyia kazi zake nchini Marekani, Edward Kakembo pamoja na lile la Desemba.