November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mtandao wa Polisi wanawake wawakumbuka wazee

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online,Nkasi

KATIKA kuelekea maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yatakayofanyika kila mwaka ifikapo Machi 8,Mtandao wa Polisi Wanawake TPF-NET wilayani Nkasi mkoani Rukwa wametoa msaada wa vitu mbalimbali vya matumizi ya nyumbani kwa wazee vyenye thamani ya zaidi ya laki tano.

Ambapo vitu hivyo ni pamoja na mifuko ya sukari,Katoni za sabuni za mche na unga,Chumvi,mafuta na vingine.

Akikabidhi vitu hivyo kwa Wazee hao Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake wa Wilaya hiyo Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Ivona Mwanga amesema wao kama polisi wanawake wanatambua mchango wa wazee katika taifa hilo na ndiyo maana wameamua kuwaona na kuwapatia vitu hivyo.

Amesema kuwa siku ya Wanawake Duniani imelenga kutambua mchango wa wanawake katika jamii huku ndani ya Jeshi la Polisi ni kukabiliana na vitendo vya ukatili kwa kuweka usawa katika mizania ya haki kwani kila mmoja ana haki ya kuishi bila kubughudhiwa bila kujali jinsi yake.

Mwanga amedai kuwa Wazee ni moja ya kundi muhimu ambalo limepigania haki mbalimbali ikiwemo na za wanawake na watoto kiasi cha sasa kila mmoja angalau anaheshimika kwa nafasi yake bila ya kujali jinsia na kuwa hayo ni maendeleo.

Mwenyekiti wa Dawati la Jinsia Anna Kisimba amesema kuwa dawati hilo ni zao la mtandao huo wa Polisi Wanawake na kwa kuzingatia kauli yao ya ‘Uzee na Kuzeeka havikwepeki ndiyo maana wakatoa kipaumbele kwa Wazee katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake duniani kwani wanahitaji busara toka kwa kundi hilo ili kufanikisha suala la usawa katika jamii.

Hivyo amewaomba kuendelea kuyasimamia maadili mema katika jamii ikiwa ni pamoja na kukemea vitendo mbalimbali vya kikatili dhidi ya wanawake na kama wazee watashiriki ipasavyo katika vita hiyo kuna uwezekano mkubwa wa vitendo vya ukatili katika jamii kutoweka.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake wa Mkoa wa Rukwa Suzana Ndotela kwa upande wake ameomba Wazee kuendelea kuwasimamia vijana wao na kutoa ushirikiano katika kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake.

Ofisa Maendeleo ya Jamii Farida Nyang’uye amewashukuru Polisi Wanawake kwa kuwatambua Wazee katika vita hiyo ya kuelekea usawa kati ya Wanawake na jinsia nyingine ya kiume kwani wote wana haki sawa katika jamii na kila mmoja anatakiwa kutekelezewa haki zote za msingi bila ya kubaguliwa kwa namna yoyote.

Mwenyekiti wa mtandao wa Wazee wilaya Nkasi kupitia shirika lisilo kuwa la kiserikali la NKANGO Jeneroza Kayanda amewashukuru Polisi kupitia mtandao wao wa Polisi Wanawake kwa kuwatambua kundi hilo kama sehemu ya jamii katika mapambano ya kutafuta usawa wa kijinsia hivyo watawaelimisha watoto juu ya umuhimu wa usawa wa kijinsia.