Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam
ZIKIWA zimesalia saa chache kabla ya Watanzania kupiga kura za kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani, baadhi ya Watanzania wanaotumia mtandao wa intaneti wamemtabiria ushindi Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt John Magufuli.
Matokeo hayo ni kwa mujibu wa kura ya maoni inayoendeshwa na tovuti maarufu ya kurayamtandaoni.com huku takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano nchini Tanzania (TCRA) za hadi kufikia Juni 2020 zikionesha kuwa Tanzania ina jumla ya watumiaji wa intaneti wapatao 27,100,146.
Mtindo huo wa kura ya maoni kwa njia ya mtandao, umekuwa kwa kasi sehemu nyingi duniani hasa kutokana na matumizi ya mtandao wa intaneti kuongezeka miaka ya karibuni na wanasayansi wengi wa siasa wanaamini kura ya maoni ya mtandao yenye sampuli yenye uwakilishi sahihi hutoa mwelekeo wa picha halisi ya matokeo ya chaguzi.
Takwimu za tovuti hiyo zinaonyesha kuwa, mpaka kufikia leo alasiri, jumla ya watu 27,877 walikuwa tayari wamepiga kura ya maoni katika mtandao huo, huku Dkt. Magufuli akipata kura 20,230 sawa na asilimia 72.57, akifuatiwa na Mgombea wa CHADEMA, Tundu Lissu mwenye kura 5,080, sawa na asilimia 18.22.
Mvutano mkubwa katika uchaguzi wa mwaka huu unatarajiwa kuwa kati ya vyama vya CCM na CHADEMA ambapo Dkt. Magufuli anagombea muhula wa pili huku akijinadi kwa kazi ya miaka mitano ya awali katika kuboresha miundombinu, upatikanaji wa umeme vijijini, afya, mabadiliko katika sekta ya elimu, nidhamu kwa utumishi wa umma na matumizi serikali.
Lakini mgombea wa CHADEMA Wakili Tundu Lissu ambaye amekuwa nchini Ubelgiji kwa kipindi kirefu akipata matibabu toka aliposhambuliwa kwa risasi mjini Dodoma, akijinadi kwa kauli mbiu ya maendeleo, haki na uhuru wa watu.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu una jumla ya Wagombea Urais 15 huku takwimu za Tume ya Uchaguzi (NEC) zikionesha kuwa, Tanzania ina wapiga kura 29,188,347, vituo vya kupigia kura 80,155 ambapo kwa Tanzania Bara kuna vituo 79,670 na kwa upande wa Zanzibar kuna ituo 1,412, hii ikiwakilisha idadi ya wapigakura 500 kwa kila kituo.
Iwapo watumiaji wa intaneti wamebashiri sahihi au la kwa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania mwaka huu, ni suala la kusubiri kuona pale matokeo yatakapotangazwa.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi