February 20, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mtanda :Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeamua kuwafikia wananchi pale walipo

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Mkuu wa mkoa wa Mwanza,Saidi Mtanda amezindua Kamati ya Ushauri wa Kisheria ya Mkoa wa Mwanza tarehe 17 Februari 2025 na kufuatiwa na Kliniki ya Sheria bila malipo kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza inayoanza Februari 17 hadi 23, 2025 katika Viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kliniki ya Sheria bila malipo kwa Wananchi wa Mkoa wa Mwanza, Mtanda amempongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali ,Hamza Johari pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa Ujumla kwa kuuchagua Mkoa wa Mwanza na kufanya Kliniki hiyo.

“Nimpongeze Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi yake kwa ujumla kwa kuuchagua mkoa wetu wa Mwanza na kuja kufanya Kliniki hii ambayo itasaidia kutatua masuala mbalimbali yanayohusu sheria”.

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, ameeleza kuwa Kliniki hiyo ni sehemu ya juhudi za Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuwafikia kwenye maeneo yao wanayoishi.

“Ofisi hii ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeamua kusogeza huduma za kisheria kwa wananchi kwa kuwatembelea wananchi kule waliko.”

Katika hatua nyingine, Mtanda ametoa wito kwa wananchi kutembelea kwenye viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili waweze kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili.

“Niwaombe wananchi wa Mkoa wa Mwanza kutumia fursa hii ya Kliniki mje mpate huduma za kisheria kutoka kwa Mawakili wetu, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeona itekeleze maono ya Rais ya kuwafikishia huduma za kisheria wananchi ambao hawana uwezo wa kupata huduma hizo.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Ushauri na Uratibu wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Neema Ringo akimuwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amesema kuwa Kamati za Ushauri wa Kisheria katika ngazi ya Mkoa na Wilaya zimeanzishwa kwa lengo la kutatua migogoro mbalimbali ya kisheria baina ya wananchi na Serikali au wananchi kwa wananchi.