January 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Baadhi ya akina mama wakimsikiliza mratibu (hayupo pichani) husiana na chakula anachostahili kupewa mtoto aliye chini ya miezi sita.

‘Msitumie maziwa ya ng’ombe kwa watoto chini ya miezi sita’

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Iringa

MGANGA Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Dkt.Jesca Leba amewataka kinamama wanaojifungua kufuata maelekezo ya wataalamu ikiwemo kutowaongezea chakula chochote hadi watakapofikisha miezi sita kwa lengo la kulinda afya za watoto hao.

Dkt.Leba ametoa rai hiyo kwenye kongamano la Mothers Meet Up event maalum kwa akina mama wanaonyonyesha lililoandaliwa na USAID TULONGE AFYA kwa lengo la kuwakumbusha kinamama hao malezi bora ya watoto ambapo amesema watoto wanaozaliwa hawapaswi kuongezewa chakula chochote kwakuwa nyongeza hiyo ya chakula uathiri afya na ukuaji wao kimwili na kiakili.

Aidha Dkt.Leba ameongeza kuwa zipo mila na desturi mbaya zilikuwa zinaathiri kampeni hiyo lakini kwa juhudi za Serikali na wadau jamii imeelewa na kuanza kufuata utaratibu huo na kuongeza kuwa kwa mujibu wa takwimu walizonazo kwa sasa unyonyeshaji bila nyongeza ya chakula kwa miezi sita ni karibu asilimia mia moja.

“Tulikuwa na changamoto ya mila na desturi katika mkoa wetu huu wa Iringa ambapo wazazi walikuwa wakishinikizwa na wanafamilia,bibi au majirani kwamba mtoto akilia anapaswa kupewa uji au hata maji kwa madai kuwa maziwa ya mama pekee hayatoshi lakini kwa sasa wengi wamekwishaelewa na utekelezaji ni karibu asilimia mia moja” anaongeza Dkt .Leba.

Baadhi ya akinamama hao wametoa ushuhuda na kueleza kuwa changamoto ya mila na desturi ilikuwa kikwazo kutokana na jamii inayowazunguka kulazimisha watoto kupewa nyongeza ya chakula ndani ya muda mfupi baada ya kuzaliwa kwa madai kuwa maziwa ya mama pekee hayawezi kumtosheleza.

“Mimi nilipojifungua ndani ya kipindi cha wiki mbili mtoto wangu wa kwanza alikuwa analia sana ndipo nikaambiwa nimuongezee chakula kwa madai kuwa maziwa yangu yalikuwa hayatoshi. Lakini nilikataa na kuendelea kumnyonyesha mwanagu mpaka alipofikisha miezi sita ndipo nikaanza kumuongezea vyakula na mpaka sasa ana afya njema” amesema Theresia Joseph ambaye ni mzazi wa watoto wawili.

Sezaria Andrew ni yeye ni Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto wa Manispaa ya Iringa amesema pamoja na hamasa iliyofanywa na Serikali katika kuhakikisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita unazingatiwa, mchango wa wadau si wakubezwa katika mafanikio yaliyofikiwa kwenye kampeni hiyo.

“Tunawashukuru wadau wetu USAID TULONGE AFYA kwani wamekuwa kiungo kikubwa kwenye kampeni hii hata kutufikisha kwenye mafanikio haya,tunawaomba waendelee kutuunga mkono ili tuendelee kumpambania mtoto wa kitanzania. Watoto wanaoanzishiwa chakula kabla ya miezi sita ya kuzaliwa wengi husumbuliwa na magonjwa mbalimbali ikiwemo magonjwa ya tumbo kutokana na utumbo kutokuwa na uwezo wa kuchakata chakula” amesema.

Mkoa wa Iringa ni moja ya mikoa yenye udumavu wa watoto ukiwa na asilimia 47 licha ya mkoa huo kuwa ni moja ya mikoa inayozalisha chakula kwa wingi jambo linaloelezwa ni kutokana na mila na desturi mbaya