Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
WAANDISHI wa Habari nchini wametakiwa kutumia kalamu zao kuandika habari zitakazosaidia kuilinda nchi na kukataa kutumia kalamu zao kuandika habari za kuvuruga tunu za taifa ikiwemo amani na utulivu.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Disemba 13,2024 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali,Gerson Msigwa wakati akikabidhiwa Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nicholaus Mkapa mbele ya waandishi hao.
Ambapo Msigwa alitumia nafasi hiyo kuwaomba Waandishi wa Habari kuendeleza ushirikiano kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kusukuma gurudumu mbele ili kumuonesha Rais Samia kuwa amefanya maamuzi sahihi ya kuihamishia Idara ya Habari katika Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Akikabidhi Idara hiyo, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Nicholaus Mkapa amesema kuwa ameikabidhi Idara ya Habari kutoka iliyokuwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambayo sasa ni Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwenda Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ikiwa na Taasisi zake tatu ambazo ni Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), na Bodi ya Ithibati.
Kwa upande wake aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali,Thobias Makoba amewashukuru Waandishi wa Habari kwa uzalendo wao wanaoendelea kuuonesha kwani bila uzalendo, kalamu ya mwandishi inaweza ikabomoa jamii huku akitolea mfano waandishi walivyoshiriki kutoa taarifa zilizo sahihi kwa jamii yalipotokea maafa ya kudondoka kwa ghorofa Kariakoo.
More Stories
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam
MSF ilivyojidhatiti kusaidia serikali katika utoaji wa huduma za afya