November 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mshindi NBC Marathon kuondoka na milioni 3.5

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

WAKATI joto la Mbio za Kimataifa za NBC Marathon zinazotarajiwa kufanyika Novemba 22 jijini Dodoma likizidi kupanda, Mshindi wa kwanza katika Mbio za Kilomita 42 kwa upande wa wanaume na wanawake ataondoka na kitita cha Sh. 3,500,000.

Mbio hizo za NBC Dodoma Marathon ambazo zinatarajiwa kushirikisha washiriki 3,000 zitajumuisha Mbio za Kilomita 42, Kilomita 21, Kilomita 10 na Kilomita 5 maarufu kama ‘Fun Run’.

Hadi sasa tayari Maandalizi wanariadha mbalimbali maarufu kutoka ndani na nje ya nchi wamekwishajisajili kuelekea mbio hizo zinazoendeshwa kwa ushirikiano kati ya Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).

Katika mashindano hayo, mshindi wa pili atajinyakulia kitita cha Sh. 2,500,000 wa tatu atapata Sh. 1,500,000, wa nne Sh. 1,000,000 huku wa tano akijitwalia Sh. 750,000 wakati watakaoshika nafasi ya sita hadi kumi kila mmoja ataondoka na Sh. 500,000.

Kwa upande wa Kilomita 21 mshindi atajipatia Sh. 2,500,000, wa pili 1,500,000 wa tatu 1,000,000, Sh. 750,000 kwa msindi wa nne na Sh. 500,000 kwa mshindi wa tano huku wale watakaoshika nafasi ya sita hadi kumi wakiondoka na Sh. 300,000 kila mmoja.

Mbio za Kilomita 10 mshindi atajitwalia kitita cha Sh. 1,000,000 wa pili Sh. 750,000 wa tatu Sh. 500.000 wa nne Sh. 250,000 wakati wa tano atajishindia Sh. 200,000 wakati wa sita hadi kumi wakijipoza na Sh. 100,000.

Kwa upande wa mbio za kujifurahisha za Kilomita 5, washiriki wote watakaofanikiwa kumaliza watajipatia medali.

Ada kujisajili ni Sh. 25,000 ambapo usajili unaendelea katika matawi ya NBC, Shoppers Plaza jijini Dodoma na Mlimani City Dar es Salaam na kila atakayejisajili atapata fulana maalumu ya kukimbilia.

Mbali na kujenga afya na kuutangaza zaidi mchezo wa Riadha, NBC Marathon pia inalenga kusaidia jamii yenye uhitaji, ambapo kwa mwaka huu mapato yote yatakayopatikana kupitia usajili yatapelekwa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kusaidia akina mama wanaosumbuliwa na kansa ya shingo ya kizazi.