Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOnline<Dar
BOHARI ya Dawa (MSD), imesema kuna haja ya kuwa na akiba ya mifuko ya kuhifadhia damu itakayodumu kwa kipindi cha kuanzia miezi mitano hadi tisa, kuepuka kuadimika kwa damu.
Kauli hiyo ya MSD imekuja katika kipindi ambacho, akiba ya mifuko hiyo kwa sasa ni miezi mitatu, jambo linalopaswa kuongezeka kutokana na ongezeko la mahitaji ya damu linalosababishwa na ajali.
Akizungumza jana wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Wataalamu wa Maabara, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, amesema MSD inaona kuna haja ya kutafuta mbinu thabiti itakayowezesha kuwa na akiba kubwa ya mifuko na hivyo kuwa na uhakika wa upatikanaji wa damu salama kwa wananchi.
Amesisitiza kuwa, damu ni suala linaloamua maisha ya watu na mahitaji yake ni muhimu hasa kwa wajawazito, hivyo kuna haja ya kuhakikisha inapatikana kwa uhakika.
Katika kufanikisha hilo, alisema kuna haja ya kuwa na akiba ya mifuko ya kuhifadhia damu itakayodumu kwa miezi mitano hadi tisa, badala ya mitatu ya sasa.
“Serikali imejitahidi kuhakikisha kunakuwa na mifuko ya kuhifadhia damu. Kwa sasa akiba inaweza kudumu kwa miezi mitatu, lakini kunahitajika collective approach (mbinu za pamoja) kukabiliana na hilo,” amesema.
Ameeleza kwa kutumia mbinu hizo za pamoja taifa litakuwa na uwezo wa akiba ya mifuko kwa zaidi ya miezi mitano na kuwezesha uhakika wa upatikanaji wa damu kwa wananchi.
“Kuna eneo bado tunaweza tukafanya vizuri zaidi ili taifa liwe na mifuko isiyopungua miezi mitano hadi tisa,” amesema.
Amesema, akiba ya mifuko iliyopo sasa ni miezi mitatu na kwamba kuna haja ya kutafuta mbinu za kuongeza akiba hiyo.
Tukai alisisitiza kuwa kikao hicho kinalenga tathmini ya utendaji katika maabara ili kuhakikisha kunakuwa na ubora wa huduma.
“Tunachotaka ni kuwa na uratibu wa pamoja na uwazi nje ya kufanya hivyo kuna watu hawataelewa kama bidhaa fulani ipo eneo fulani,” amesema.
Lakini hatua hiyo, alisema itawezesha kupunguza kuisha muda wa baadhi ya vifaa kabla ya kutumika, ilhali kuna taasisi zinazohitajika.
“Tunataka kupunguza ile hali ya vitendanishi kuisha muda wake kabla ya kutumika ilhali kuna maeneo vilikuwa vinahitajika ila tu hawakuwa wanajua,” amesema.
Naye Kaimu Mfamasia Mkuu wa serikali, Msafiri Chiwanga, alisema serikali imeendelea kuwekeza katika mashine za kiuchunguzi ili kuhakikisha mgonjwa anapatiwa tiba sahihi kulingana na ugonjwa unaomsumbua kupitia kwa wataalamu wa maabara.
Amewataka wataalamu hao kuhakikisha wanafanya kazi kwa kuzingatia kanuni na sheria kulingana na miongozo iliyowekwa ili huduma inayotolewa iweze kuwa na ubora unaokubalika katika sekta ya afya.
Amesema, kufuatia kuwepo kwa changamoto za usugu wa vimelea vya magonjwa katika baadhi ya dawa, wataalamu wa maabara wanatajwa kuwa msaada katika kuhakikisha tiba inayotolewa kwa mgonjwa inaendana na ugonjwa husika na hii ni baada ya matokeo ya vipimo kupitia mashine za kiuchunguzi.
More Stories
Watakiwa kushirikiana kutikomeza matatizo ya lishe
CCBRT yazidi kuunga mkono juhudi za Rais Samia
Madaktari bingwa wa Samia watua Rukwa