Na Stella Aron,TimesMajira Online, Dar
BOHARI ya Dawa (MSD) imefanikiwa kuanzisha viwanda saba nchini vitakavyozalisha dawa na kusaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa dawa nchini ikiwa ni pamoja na kuendana na kasi ya Serikali uboreshaji huduma ya afya nchini.
Akizungumza katika semina ya waandishi wa habari iliyofanyika jana Dar es Salaam,Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa(MSD), Meja Jenerali Gabriel Mhidzewame amesema kuwa kati ya viwanda hivyo kipo cha barakoa, vitakasa mikono, dawa za rangi mbili na dawa za vidonge.
Amesema kuwa MSD imefanya jitihada kubwa za kuhakikisha kuwa uzalishaji wa mipira ya mikono ‘gloves’ unafanyika nchini katika kiwanda kilichopo Idofi mkoani Njombe ambacho kinatarajiwa kuanza uzalishaji wa bidhaa hizo ifikapo Novemba mwaka huu.
Amesema kuwa kiwanda hicho kitasaidia kupunguza gharama za kuagiza mipira hiyo kutoka nchi za nje ambayo kwenye soko la dunia imepanda kutoka dola 3.4 mwaka jana hadi kufika dola 12 kutokana na janga la ugonjwa wa Uviko -19.
“Kuanzia Novemba Watanzania watarajie kupata gloves zinazotengenezwa hapahapa nchini, jambo ambalo tuna imani litapunguza gharama ya kuagiza bidhaa hizi nje ya nchi,’ amesema.
Pia amesema kuwa viwanda hivyo vitakuwa vikizalisha pia mafuta ya ngozi yakiwemo ya watu wenye ualbino huku matarajio yakiwa ni kuzalisha na dawa za mswaki.
Akizungumzia mafanikio mbalimbali yaliyopatikana MSD Meja Jenerali Mhidze amesema kuwa pia kutatengenezwa dawa za maji (syrup) na za vidonge vya unga na zile za rangi mbili.
Vilevile, Meja Jenerali Mhidze amesema wanatoa huduma ya mashine za kupimia magonjwa mbalimbali ambazo watazigawa kulingana na daraja la hospitali kwani malengo yao ni kadri Serikali inapoongeza vituo vya afya na hospitali kuhakikisha wanafikisha huduma hiyo.
Pia amesema kwa kutambua umuhimu wa huduma ya uchujaji damu, wameamua kuleta mashine za kuchuja damu kwa gharama nafuu ili wananchi wapate huduma kwa gharama nafuu.
“Tutakwenda na kasi ya Serikali katika ujenzi wa vituo vya afya kwa sisi kuufikisha mashine hizo ili ziendelee kutoa huduma.Tumeona upo umuhimu wa kushirikiana na wafanyabiashara ili kuongeza fursa ya utoaji huduma bora kwa wananchi na mipango tuliyonayo haina nia ya kuua biashara ya wafanyabiashara,”amesema.
Naye msimamizi wa Viwanda vya Idofi, Selwa Hamid, amesema kuna mafanikio mengi ambayo yamepatikana MSD ikiwa ni kuboresha huduma za afya nchini hivyo kukamilika kwa viwanda hivyo kutasaidia kupunguza gharama kubwa ambayo Serikali ilikuwa ikitumia kwani vitakuwa na uwezo wa kuzalisha gloves 20,000.
“Tuna uwezo wa kuzalisha jozi 10,000 kwa siku kwa maana ya gloves 20,000 hivyo tuna uwezo wa kuhudumia nchi na pia kuhudumia nchi zingine hasa katika makubaliano tuliyonayo wa kusambaza dawa na vifaatiba nchi za SADC,” amesema.
More Stories
Wananchi Babati wamshukuru Rais Samia kwa kuwafungulia barabara
Rais Samia aungwe mkono ajenda ya nishati safi ya kupikia
Ushiriki wa Samia G20 wainufaisha Tanzania