December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Msama awashauri waandaaji matamasha

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online Tabora

Mkurugenzi wa Msama Promotion, Alex Msama amewashauri waandaaji wa matamasha ya injili kutofanya tamsha kama biashara, bali wafanye tamasha kama huduma kwa lengo la kupokea baraka za Mwenyewezi Mungu.

Msama ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam katika Kipindi Cha Gospel Celebration na kusema kuwa huduma hiyo hatoiacha na ataendelea kuitoa kama huduma.

“Wanaofanya matamasha, wasiingie kwa lengo la biashara, wasiingie kwa lengo la kusema watapata pesa”

“Matamasha kwangu mimi ni huduma na siyo biashara, kwahiyo ukija kibiashara huwezi kurudi tena, ndiyo maana huduma hii nimeianza mda mrefu lakini kwangu mimi huduma hii imekuwa na mafanikio makubwa na baraka kubwa kwangu, wengi hawaamini kwamba mungu anabariki” Ameongeza Msama

Msama amesema kutokana na ufanyaji wake wa tamasha bure, baraka na utukufu unatawala katika shughuli zake nyingine ikiwemo kuongezeka kwa kipato katika biashara zake.

“Biashara zangu nyingine mungu anazibariki, ananiinua na kunipigania, na kuinua kipato changu katika shughuli zangu, kuna mambo mengi ambayo nayaona kwenye maisha yangu hivyo nikaona njia pekee ya kumshukuru Mungu ni kumtumikia yeye kuhakikisha kwamba anapewa sifa na namtangaza kuwa yupo na anastahili kupewa sifa na utukufu”

Amesema tamasha la mkesha wa pasaka ametumia milioni 150 lakini baada ya kumaliza tamasha hilo ameona baraka nyingi za mungu zikimfikia.

Pia amesema amefanya tamasha katika viwanja vya leaders bure, na kuleta waimbaji wengi kutoka Kongo, Kenya na nchi nyingine kwaajili ya kutumbuiza katika tamasha hilo.

“Huduma hii ya tamasha siiachi naendelea nayo, wengi wanaofanya tamasha kibiashara wanakuja na hawarudi tena wanaishia kugombana, wengi wao wanajuta kwanini wamefanya ,Mimi sijutii kwasababu naziona baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hii ni huduma ambayo ipo ndani ya moyo wangu”

“Matamasha siyaachi kwasababu nimemwambia Mungu kwamba nitamtumikia kwa njia ya matamasha, nitamtangaza yeye kwamba yupo Kila kona ya Taifa letu”

Mbali na hayo Msama amewataka wananchi kuwa tayari kupokea jambo lingine kubwa ambalo analiandaa ndani ya mwaka huu.”Kwa mwaka huu wananchi wategemee lolote, kuna mambo ambayo tunayaandaa kwaajili ya kuhakikisha kwamba mwaka huu tunafanya kitu kwaajili ya kumtukuza Mungu na kumsifu”