January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Msako siku 13 wanasa watuhumiwa 200

Judith Ferdinand,TimesMajira Online, Mwanza

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza katika kipindi cha siku 13, limefanikiwa kufanya msako na kuwakamata watuhumiwa 264 kwa tuhuma za kuhusika na makosa mbalimbali.

Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa,jijini Mwanza,ambapo ameeleza kuwa jeshi hilo
limeendelea kuimarisha hali ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Mwanza kwa kufanya misako na doria mbalimbali na kufanikiwa kukamata watuhumiwa hao.

Mutafungwa ameeleza operesheni hiyo ilianza Aprili 1 hadi Aprili 13 mwaka huu katika maeneo mbalimbali mkoani hapo hivyo kuwakamata watuhumiwa hao na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Ameeleza kuwa miongoni mwa matukio ni pamoja na lillilotokea Apri13.04.2023 muda wa saa 2, huko katika Kata ya Magu mjini, Tarafa na Wilaya ya Magu, katika barabara ya Mwanza/Musoma, Gari namba T.826 DKK,aina ya Mazda Primas, mali ya Beatus Francis @Chiganga, lilikamatwa likiwa na viroba tisa (9) vya mirungi inayokadiriwa kuwa na uzito wa zaidi ya kiloagram 70.

Ameeleza kuwa awali gari hilo kabla ya kukamatwa liligonga kizuizi cha magari na kupoteza uelekeo kisha kugonga mti, baada ya tukio hilo dereva alikimbia na kwenda kusiko
julikana.

“Baada ya upekuzi katika Gari hilo Askari walikuta viroba tisa vya mirungi na
kufanikiwa kuvifikisha kituo cha Polisi Magu pamoja na gari hilo lililokuwa
limepata uharibifu wa kupasuka tairi tatu, tunaendelea kumsaka dereva wa gari hilo kwa tuhuma za kusafirisha dawa hizo za
kulevya aina ya mirungi ili aweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,”.

Pia Aprili,6,2023, Kata ya Buswelu,
Tarafa na Wilaya ya Ilemela, Askari wakiwa doria walimkamata Jackson Mussa,(22)mkazi wa Bujingwa pamoja na wenzake wawili wakiwa na
gramu 69.3 za dawa za kulevya aina ya mirungi.

Ambapo Watuhumiwa wote wamehojiwa
na watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Katika msako huo Aprili,8,.2023, katika Kitongoji cha Mantale, Tarafa ya Nyanguge, Wilaya ya Magu, Askari wakiwa doria walifanikiwa kuwakamata Kulwa Makoye(43) mkulima na mkazi wa Nyanguge na Batina Felishian(47) mkulima na mkazi wa Nyanguge wakiwa na mafuta ya diesel lita 160 yadhaniwayo kuwa ni mali ya wizi.

Pamoja na mapipa 4 matupu ya lita 200,
madumu 40 matupu, mpira wa kunyonyea mafuta na nondo 18 za mm18, ambazo
zilikuwa zimehifadhiwa nyumbani kwa Daudi Shija(23) mkulima na mkazi wa Kijiji cha Maligisu kinyume na sheria ambapo watuhumiwa wamehojiwa na
kufikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.

Tukio jingine lilitokea Machi 31,2023 muda wa 01:00 huko Kitongoji cha Kanyama Magharibi, Kijiji cha Kanyama, Kata ya Bujora, Tarafa ya Sanjo, Wilaya ya Magu, Askari wakiwa doria walimtilia shaka na kumkamata Saidi Fikirini(21) mkazi wa Kanyama.

Baada ya kumpekua alikutwa akiwa na simu za aina mbalimbali tisa, kifaa cha kusajilia line na line mpya saba kampuni ya TTCL mali idhaniwayo kuwa ya wizi,mtuhumiwa alihojiwa na tayari ameshafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi.

Vilevile Aprili 03,2023,Kata ya Mirongo, Wilaya ya Nyamagana, Askari wakiwa doria walimkamata Alex Guido(33) Mkazi wa Caprpoint na Baraka Richard, miaka (18) mkazi wa Mkuyuni na baada ya
kupekuliwa kwenye kibanda chao cha kuuzia mahitaji madogo madogo ya nyumbani, walikutwa na mifuko ya plastiki pisi 96 iliyopigwa marufuku na serikali hivyo watuhumiwa watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi.

Akizungumzia upande wa usalama barabarani katika kipindi cha wiki mbili kuanzia Aprili 1 hadi Aprili 13 mwaka huu Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza,limefanikiwa kudhibiti
matukio ya ajali barabarani kwa kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria madereva 13 waliovunja sheria za usalama barabarani.

Ambapo makosa ya ajali yaliyoripotiwa ni 2, idadi ya watu waliofariki kutokana na ajali ni 2, majeruhi 3 ukilinganisha na kipindi hicho mwezi uliopita ambapo makosa ya ajali yalioripotiwa yalikuwa 3, idadi ya watu waliofariki kutokana na ajali ni 2 na
majeruhi walikuwa 5.

Ameeleza kuwa mafanikio hayo yote yametokana na elimu inayoendelea kutolewa kwa makundi mbalimbali ya watumiaji wa barabara ambapo kupitia radio, mitandao ya kijamii,magazeti na television wananchi wameendelea kuelimishwa juu ya masuala
mbalimbali ya usalama barabarani.

“Stendi za mabasi,vyuo vya udereva,
kanisani, vijiwe vya bodaboda, shule pamoja na vyuo, hayo ni baadhi ya maeneo ambayo elimu imeendelea kutolewa kwa lengo la kudhibiti ajali za barabarani,”.

Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kupitia mpango mkakati wa kushirikisha jamii katika hali ya kutanzua na kuzuia vitendo vya kihalifu limefanikiwa kutoa elimu kwa jamii jinsi ya kuzuia na kupambana na uhalifu katika maeneo
mbalimbali.

Ambapo mikutano 129,mashindano ya Polisi Jamii cup, 2023 yenye lengo ya kuiweka jamii pamoja yanaendelea kwa kuwakutanisha vijana wa kata 37,yamefikia katika hatua ya robo fainali.

Sambamba na jitihada hizo wakaguzi wa Kata za Mkoa wa Mwanza wanaendelea
kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya usalama katika kata zao kwa
kushirikisha makundi mbalimbali kupitia mikutano, vikao shuleni, kanisani,
misikitini, kwa waganga wa tiba asili, wamiliki na walinzi wa makampuni binafsi ya
ulinzi ili kuweza kudhibiti vitendo vyote vya uhalifu.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linaendelea kutoa rai kwa wananchi kuendelea
kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili ziweze kufanyiwa kazi kwa wepesi na
haraka.

Pia linawakumbusha madereva kufuata sheria za usalama barabarani kwa
kuzingatia elimu inayotolewa kwao ili kumaliza kabisa tatizo la ajali za barabarani.