Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Taasisi na mashirika ya umma nchini yametakiwa kutumia fursa zinazotolewa na Benki ya CRDB kwa ajili ya kuongeza ufanisi na tija. Rai hiyo imetolewa na Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto katika semina maalum iliyoandaliwa na benki hiyo na kuwaleta pamoja wakuu wa taasisi, mashirika na wakala za Serikali.
Akizungumza katika semina hiyo iliyofanyika katika hoteli ya Johari Rotana Jijini Dar es Salaam, Mgonya amesema ili taasisi,Wakala, na mashirika hayo kuendana na kasi na malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita kunahitajika ufanisi wa kifedha ambao utasaidia kuboresha utendaji na huduma wanazozitoa kwa wananchi.
“Benki ya CRDB imetudhihirishia hapa utayari wake wakushirikiana na taasisi, mashirika na wakala zetu katika kuboresha ufanisi kupitia huduma na bidhaa bunifu zinazotolewa na benki hii. Tuitumie fursa hii vizuri kwani benki hii ina uwezo mkubwa wa uwezeshaji wa kimifumo na kifedha kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia katika miradi ya kimkakati,” aliongezea Mgonya.
Aidha, Mgonya alibainisha kuwa Serikali imeweka mkakati madhubuti wa kuhakikisha taasisi, mashirika, na wakala za Serikali zinaleta tija kwa Taifa. “Mkakati huu umekuwa na manufaa kwa Serikali kwani katika Mwaka wa Fedha wa 2021/22 ulioishia Juni 30, Ofisi tumefanikiwa kukusanya mapato yasiyo ya kodi ya jumla ya Sh bilioni 852.98 ikiwa ni asilimia 109.50 ya lengo.”
Serikali ina uwekezaji katika taasisi na mashirika 297, wenye thamani ya Sh. trilioni 67. “Moja ya hizo ni Benki ya CRDB. Tunajivunia utendaji wake ambapo kila mwaka imekuwa ikitupa gawio, ambapo punde tu wametupa gawio la Sh. bilioni 36.1. Niwapongeze sana, na pia niwapongeze kwa namna ambavyo wamedhamiria kuzijengea uwezo taasisi, mashirika, na wakala zetu za Serikali,” alihitimisha.
Akiwasilisha mada katika semina hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alimhakikishia Msajili wa Hazina kuwa Benki hiyo ipo tayari kufanyakazi kwa ukaribu na taasisi, mashirika, na wakala za Serikali ili kuongeza ufanisi katika utendaji wao, kuboresha huduma kwa Watanzania, na kuongeza tija ya mchango wao katika mapato ya Serikali.
“Semina hii ni mwitikio wa wito wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wakuzitaka taasisi za umma kushirikiana na taasisi binafsi ili kuboresha utendaji na kuleta tija zaidi kwa Watanzania. Tukiwa ‘Benki ya Kizalendo’ hili ni eneo ambalo tumelipa kipaumbaule na malengo yetu ni kujenga ushirikiano ambao utaziongezea taasisi za Serikali ufanisi wa kifedha,” alisema Nsekela.
Akielezea maeneo ambayo benki hiyo imejipanga kushirikiana na taasisi za Serikali, Nsekela alisema Benki ya CRDB ina mtaji wa kutosha kuwezesha miradi, na programu za maendeleo zinazotekelezwa na taasisi hizo. Aliongezea kuwa benki hiyo pia ina huduma za uwekezaji, pamoja na mifumo thabiti ya kusaidia ukusanyaji wa mapato na kufanyia malipo.
“Benki yetu pia inahuduma kwa ajili ya wafanyakazi wa taasisi na mashirika haya zinazolenga kusaidia kuboresha maisha yao. Tuna huduma za akaunti za mishara, huduma za uwezeshaji kupitia mikopo, na huduma za kidijtali ambapo hivi sasa mfanyakazi anaweza kupata mkopo popote pale alipo kidijitali kupitia huduma ya ‘Salary Advance’ inayopatikana katika SimBanking,” alisema.
Akiongea kwaniaba ya taasisi, mashirika na Wakala za Serikali zilizohudhuria semina hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), Abdulrazak Badru ameishukuru Benki ya CRDB kwa kuandaa semina hiyo ambayo imetoa fursa ya kujadili changamoto zinazozikabili taasisi na mashirika ya umma nchini, pamoja na fursa zinazotolewa na benki hiyo.
“Bodi ya Mikopo ni moja ya washirika wakaribu wa Benki ya CRDB kupitia mfumo wa usajili na utoaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ambao umetusaidia kuongeza ufanisi katika utoaji mikopo. Tunajivunia ushirikiano huu, na leo hii tumepata kujifunza fursa na maeneo mengine ya ushirikiano ambayo naamini yataongeza tija katika taasisi yetu,” alisema Badru.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi