November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza (Picha na Maktaba)

Msajili: Makao makuu ya vyama yawe Dodoma

Na Mwandishi Wetu – ORPP

OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ametoa wito kwa vyama vya siasa kufungua ofisi za makao makuu Jijini Dodoma kwa kuwa ndiyo Makao Makuu ya Serikali.

Wito huo umetolea na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, alipotembelea ofisi ndogo za Makao Makuu ya Chama cha Wakulima (AAFP) jijini Dodoma hivi karibuni.

Nyahoza alisema kuwa vyama vyote vya Siasa vinatakiwa kuwa na ofisi za makao makuu jijini Dodoma kwa kuwa ndiko shughuli zote za Serikali zinapofanyika kutokana na Serikali kuhamishia makao makuu yake jijini humo.

“Natoa wito kwa vyama vingine vya siasa ambavyo havina ofisi ndogo za makao makuu jijini Dodoma kufungua ofisi zao ukizingatia kuna vyama vya siasa ambavyo vinapata ruzuku ya Serikali ninategemea viwe na ofisi bora na nzuri hapa Dodoma kwa sababu uwezo huo wanao”, alisema Nyahoza.

Aliongeza kuwa awali vyama vya siasa vilifungua ofisi zao jijini Dar es Salaam kwa kuwa shughuli za kiserikali zilikuwa huko kabla ya kuhamishiwa Dodoma ambapo ndio makao makuu.

“Kama ambavyo mlienda kufungua ofisi za vyama vya siasa jijini Dar es Salaam kutokana na kuwa karibu na ofisi za Serikali, natoa wito sasa kwa vyama hivyo kuja Dodoma na kufungua ofisi zao kwakuwa huku ndiko makao makuu ya nchi na Serikali”, alisisitiza Nyahoza.

Katika hatua nyingine, Nyahoza, amevitaka vyama vya siasa nchini kuunga mkono juhudi za Serikali katika kupambana na maambukizi ya ugonjwa COVID -19 unaosambazwa na virusi vya Corona.

“Kuna vyama vingine sasa hivi vinajiandaa kufanya mikutano mikuu ya kitaifa ya uchaguzi tunaomba hili jambo walizingatie kabisa kama ikiwezeka waahirishe mikutano kuepuka kuleta mikusanyiko kinyume na maelekezo ya Serikali badala yake wasogeze mbele mikutano hiyo.” Aliongeza Nyahoza.

Ziara hiyo ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutembelea ofisi ndogo za makao makuu ya vyama vya siasa zilizoko makao makuu ya nchi jijini Dodoma ni muendelezo wa zoezi wa uhakiki wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu lililoanza Machi 17, mwaka huu.