Asisitiza utekelezaji wa agizo la Dkt.Biteko la ufungaji mitambo ya umeme Jua
Na Mwandishi wetu, Timesmajira
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba leo ameongoza Menejimenti ya Wizara ya Nishati kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Wizara hiyo katika Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma.
Akiwa katika jengo hilo alielezwa na Msimamizi wa ujenzi wa jengo kutoka Wizara ya Nishati, Alphonce Kilovele kuwa, ujenzi umefikia asilimia 84.3 na kwamba ifikapo mwezi Januari 2025 litakuwa tayari kwa matumizi.
Kilovele ameieleza Menejimenti ya Wizara ya Nishati kuwa, kazi zinazoendelea sasa ni za umaliziaji wa huduma saidizi ikiwemo miundombinu ya umeme, maji, zimamoto, Tehama, viyoyozi na vioo.
Amesema kuwa, jengo hilo litakalochukua watumishi 200 hadi 300 linafungwa mifumo ya umeme inayozingatia matumizi bora ya Nishati (energy efficiency) ikizingatiwa kuwa Wizara ya Nishati ni kinara wa usimamizi wa matumizi bora ya nishati nchini.
Katika ziara hiyo, Mhandisi Mramba amewakumbusha wasimamizi wa jengo hilo kuhakikisha kuwa agizo la Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko la majengo yote ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake kufungwa mifumo ya nishati jadidifu ikiwemo umeme Jua linazingatiwa.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato