December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mrajis ahamasisha wakulima Tabora kutumia zana bora za Kilimo


Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

VIONGOZI wa vyama vya ushirika (Union) na vyama vya msingi vya wakulima (AMCOS) Mkoani Tabora wametakiwa kuchangamkia mradi wa matumizi ya zana bora za kilimo ili kuleta tija kubwa katika shughuli zao.

Hayo yamebainishwa jana na Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoani hapa Venance Msafiri alipokuwa akiongea na Wenyeviti na Makatibu Meneja wa Amcos na Viongozi wa vyama vya ushirika kutoka Wilaya za Urambo na Kaliua.

Alisema wakulima wengi Mkoani humo bado wanatumia zana za kizamani kutekeleza shughuli zao, hali inayopeleka kutumia gharama kubwa na muda mwingi katika kutekeleza shuhguli zao.

Alisisitiza kuwa mradi huo ni fursa muhimu sana kwa wakulima hivyo akawataka Viongozi walioshiriki mafunzo hayo kwenda kuhamasisha wanachama wao  wenye uwezo kuchangamkia mikopo ya zana hizo. 

Msafiri alibainisha kuwa matumizi ya zana bora huleta ufanisi na kuongeza uzalishaji wa mazao ya wakulima, hivyo akawataka kubainisha wanachama walio tayari kukopeshwa zana hizo za trekta ili kunufaika kazini.

Mbali na kuongeza mapato ya wakulima alisema halmashauri nazo zitanufaika na mradi huo kupitia tozo za ushuru huku akibainisha kuwa mikopo ya kununuliwa zana hizo itatolewa na benki zilizoingia mikataba ya kukopesha wakulima.

Mwakilishi wa Kampuni ya VJ Tractors and Implements Kanda ya Kati na Ziwa ambao ndio wauzaji wa zana hizo, Petro Seth alisema kupitia mradi huo wakulima watakaokidhi vigezo watapewa trekta zenye ubora wa hali ya juu na vifaa vyake.

Aliongeza kuwa dhamana ya mkulima kupata zana hizo ni chama chake cha msingi na kila atakayehitaji atachukua mkopo benki ya CRDB, NMB au Azania kwa ajili ya kulipia zana hizo na atatakiwa kurejesha mkopo huo ndani ya muda uliopangwa kupitia Amcos yake.

Aliongeza kuwa Kampuni hiyo itatoa ofa ya mafunzo kwa watumiaji juu ya namna ya kuendesha trekta hizo kwa kila atakayenunua na matarajio yao ni kuwa zitatoa ajira kwa vijana watakaozi opareti.

Katibu Meneja wa Chama Cha Msingi Nsanjo, Tausi Kiswagala alisema mradi huo utawasaidia kuachana na zana za kizamani hivyo kuboresha shughuli zao.

Aidha aliongeza kuwa utawasaidia kupunguza muda wa kuandaa mashamba na kuachana na vitendo vya utumikishwaji watoto mashambani.

Mwenyekiti wa Amcos ya Mwamakole, Wilayani Urambo Ibrahimu Kagete alisema kupitia mradi huo wataongeza ukubwa wa mashamba na kuongeza kilo zaidi za tumbaku.

Alimpongeza Mrajis wa Mkoa kwa dhamira yake njema ya kuwainua wakulima ila akashauri Wakurugenzi wa halmashauri kushirikishwa kwa kuwa wao ndo wenye dhamana ya kutoa maeneo zaidi ya kilimo.

Hamis Katabanya, mkulima mkazi wa kata ya Ugunga Wilayani Kaliua ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha msingi Tuombe-Mungu alisema mradi huo utawasaidia kuachana na kilimo cha mazoea na kufanya kilimo cha biashara.

Alisema kama walilima kwa zana duni na kupata hela sasa watakuwa matajiri kwa kuwa watarahisisha shughuli zao na kuongeza ukubwa wa mashamba yao.

Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoani hapa Venance Msafiri (aliyevaa tisheti ya bluu) akipata maelezo ya zao la tumbaku kutoka kwa mkulima wa Kijiji cha Tuangoma, kata ya Ugunga, Wilayani Kaliua Hamis Katabanya alipotembelea mashamba ya wakulima wilayani humo jana. Picha na Allan Vicent.
Â