Na Penina Malundo,Rusumo
HALI ya Umeme kwa nchi ya Tanzania, Rwanda na Burundi ,inaelekea kuimarika baada ya mradi wa ujenzi wa umeme katika maporomoko ya Mto Rusumo mpakani mwa nchi hizo kufikia asilimia 99.9 ya ukamilikaji wake na kuanza usambaza katika nchi hizo.
Akizungumza mwishoni mwa wiki Kigali nchini Rwanda na waandishi wa habari kutoka nchi sita, ikiwemo Tanzania, Kenya, Burundi, Rwanda, Kongo na South Sudan, Meneja Mradi wa Kanda kutoka Nile Equatorial Lakes Subsidiary Action Program Coordination Unit (NELSAP -CU), Mhandisi,Dkt. Issac Alukwea amesema mradi huo kwa sasa umefikia hatua nzuri.
Amesema tayari jenereta mbili zimeanza kuzalisha umeme katika mradi huo na kufikisha katika gridi za taifa za nchi hizo.
Amesema jenereta moja lililobaki kwa sasa lipo katika hatua ya majaribio, ambapo limeunganishwa umeme kutoka katika eneo la mradi hadi katika gridi Kuu ya Taifa la Tanzania (Nyakananzi)na lipo chini ya uangalizi wa kipindi cha mwezi mmoja.
Dkt. Alukwea amesema umeme utakaozalishwa na chanzo hicho cha maji katika maporomoko hayo utakuwa wa megawati 80 ambapo kila nchi ikiwemo Tanzania, Rwanda na Burundi zitaweza kupata megawati 27 kutoka katika chanzo hicho.
“Mradi huu uliopata fedha kutoka Benki ya Dunia kupitia taasisi ya Nile Basin Initiative (NELSAP),kupitia Kitengo cha Kodi za Kimataifa (Internation Development Taxiation walikubali kufadhili huu mradi na kuweka mkataba na mataifa yote matatu,”amesema na kuongeza;
“Huu ufadhili wa World Bank uligawanyishwa kwa kila nchi, ambapo Burundi walipewa ruzuku,Tanzania walipatiwa Mkopo na Rwanda walipewa nusu mkopo na nusu ruzuku, Nelsap walipewa kibali cha kuwa Shirika la kutekeleza mradi huo kupitia mkataba ulioitwa Project Implementation and Support Agreement,”amesema.
Dkt.Alukwea amesema mbali na fedha hizo za Benki Kuu ya dunia pia nchi hizo ziliweza kupata fedha kutoka benki ya Afrika, ambayo nayo ilikubali kufadhiri mradi huu kwenye nyaya za kusafirisha umeme.
Kwa Upande wake Meneja wa mradi wa kufua umeme wa Rusumo, Mhandisi Aloyce Oduor, amesema mradi huo utakapokamilika utaweza kuwa na faida kubwa kwa nchi hizo tatu hata kwa majirani wa nchi hizo kwa kupata fursa ya kuwa na umeme mwingi na kuweza kufanya biashara kwa nchi nyingine.
Amesema hadi sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia 99.9 ambapo umeme unaenda katika kila nchi hizo ni umeme wenye nguvu kubwa ambao unafika katika gridi za mataifa hayo.
Naye Mhandisi wa Umeme katika Kituo hicho,Mhandisi Caritace Mnampo alisema kutokana na uhaba wa umeme mradi huu utakapo kamilika utasaidia nchi hizo tatu kunufaika kwa kiasi kikubwa.
”Umeme megawati 27 sio kitu kidogo ni kubwa hatuwezi kusema utamaliza tatizo la kukatika kwa umeme ila utapunguza kwa kiasi kikubwa na mfano kwa Tanzania mradi wa Mwalimu Nyerere Hydropower utakapokamilika utapunguza sana tatizo la umeme,”amesema na kuongeza;
“Sasa ni wakati wa wananchi kuwa na imani na nchi zao kwa kuhakikisha tatizo hilo la umeme linaenda kuisha,”amesema.
Mradi huo unatekelezwa kwa kuzingatia makubaliano ya Kiserikali ya nchi za Tanzania,Rwanda na Burundi baada ya kuingia makubaliano rasmi mwaka 2012 na kutoa ajira zaidi ya 1000 kwa nchi zote tatu na nchi jirani.
Mradi unatekelezwa chini ya Wakandarasi wanne ambao wawili kutoka China ,Kampuni ya CGCOC Group na Kampuni ya Jiangxi Water & Hydropower Construction ambao wamejenga bwawa la maji pamoja na miundombinu mingine na Muunganiko wa Wakandarasi Andritz Hydro GmbH ya Ujerumani na Kampuni ya Andritz Hydro PVT ya nchini India ambo wanahuzika na ufungaji wa mitambo ya kuzalisha na kusambaza Umeme.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa