Na Esther Macha,Timesmajira,Online,Kyela
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2021, Luteni Josephine Mwambashi ameridhishwa na utekelezaji wa mradi wa maji Mababu wilayani Kyela mkoani Mbeya na kuagiza mwishoni mwa mwezi huu mradi huo ukamilike na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Luteni Mwambashi ameyasema hayo jana mara baada ya Mwenge wa uhuru kutembelea mradi huo kwa lengo la kukagua utekelezaji wake.
“Mradi huu ulipitiwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru Mwaka 2019. Leo tulikuja kuangalia hatua iliyofikiwa na kujiridhisha iwapo unatekelezwa katika viwango vilivyokusudiwa, tumeridhishwa na utekelezaji hivyo hadi mwishoni mwa mwezi huu mradi huu uwe umakamilika na wananchi wapate huduma ya maji,” amesema Luteni Mwambashi.
Aidha, kiongozi huyo amewataka wananchi kuhakikisha wanalinda miundombinu ya maji ili isiharibiwe.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi ambaye pia ni mbunge kupitia viti maalumu wanawake mkoa wa Mbeya amemhakikishia kiongozi huyo kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati.
Amesema mradi huo ulikuwa na vituo vitano vya kuchotea maji, Serikali chini ya Rais Samia iliongeza fedha kiasi cha sh. milioni 207 ambazo zimewezesha kuongeza miundombinu ya mabomba, tenki la kuhifadhia maji pamoja na vituo vinne zaidi vya kuchotea Maji kutoka vitano vilivyokuwa katika bajeti ya awali.
Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini Wilaya ya Kyera Mhandisi, Tanu Deule amesema mradi huo unatarajia kuhudumia wakazi 5,121 kutoka vitongozi vitano vya kijiji cha Mababu ambapo gharama ya utekelezaji inatarajiwa kuwa zaidi ya shilingi milioni 398.
Mwenge Maalumu wa Uhauru uko mkoani Mbeya ukitarajia kukamilisha mbio zake kesho.
More Stories
Balozi Nchimbi kuongoza waombolezaji mazishi ya Kibiti leo
Dkt.Tulia,apewa tano kuwezesha wananchi
Nkasi yajipanga kukusanya mapato