January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi wa Maji Kilindi wakamilika

Na Yusuph Mussa,TimesMajira Online

HATIMAYE Mradi wa Maji unaohudumia vijiji vya Kigwama na Muungano, Kata ya Msanja Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga umewafanyiwa marekebisho, na sasa wananchi wa vijiji hivyo zaidi ya 6,212 watanufaika na mradi huo.

Mradi huo ambao ulikuwa uzinduliwe Juni 3, 2021, Kiongozi wa Mwenge Maalumu wa Uhuru, Josephine Mwambashi alikataa kuuzindua kwa madai haujakamilka sababu baadhi ya sehemu maji safi yalikuwa yanachanganyika na tope, hivyo kuwa kero kwa wananchi.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Kilindi Mhandisi Alex Odena alisema, sababu ya kutokea tatizo hilo ni baadhi ya watu wasio waaminifu kuweza kupasua bomba kwenye maeneo ya viungio (Valvu), hivyo ikafanya maji safi kuchanganyikana na maji ya mvua yenye tope.

“Tatizo kubwa lililosababisha maji safi kuchanganyika na maji yenye tope na kufanya mabomba kutoa maji yenye tope ndani, ni kutokana na baadhi ya watu kupasua kwenye viungio. Hivyo kufanya maji ya mvua kuingia kwenye mfumo wa maji safi, na kusababisha mabomba kutoa maji yenye tope,” amesema Odena.

Mradi wa maji safi na usafi wa mazingira uliotekelezwa na Serikali Kuu, chanzo cha maji cha mradi huo ni bwawa lenye urefu wa mita 151, upana wa mita 47.2, kina cha mita 7.2 na ujazo wa 72,076M3

Ujenzi wa Mradi huo uligawanyika katika awamu mbili yaani ujenzi wa tuta la bwawa na ujenzi wa miundombinu ya kusambaza maji katika vijiji vya Kigwama na Muungano. Ujenzi wa bwawa kama chanzo cha maji ulikamilika mwaka wa fedha 2014/2015 ambapo kiasi cha sh. 418,089,644 kilitumika kujengwa bwawa la maji kama chanzo.

Odena amesema, ujenzi wa mradi kwa awamu ya pili ulianza mwaka wa fedha 2017/2018. Kazi kuu zilizotekelezwa katika awamu hiyo ni pamoja na ujenzi wa machujio ya maji, birika la kutunzia maji, nyumba ya kuhifadhia mitambo ya kusukuma maji, matenki ya kuhifadhia maji yenye ujazo wa lita 50,000 na lita 25,000, vituo 17 vya kuchotea maji, mtandao wa bomba za kupandisha maji kwenye tenki na kuyasambaza kwa watumiaji jumla ya umbali wa kilomita 13.088 na mbauti moja. Ujenzi wa miundombinu ya kusambaza maji ulikamilika Machi, 2019 ambapo kiasi cha sh. 735,940,340 kilitumika.

Mradi huo ulikadiriwa kugharimu kiasi cha sh. 1,288,310,468. Hadi Kukamilika kwa mradi huo umegharimu sh. 1,154,029,984, ambapo kumewezesha wananchi wapatao 6,212 kunufaika na huduma ya maji sambamba na kuongezeka kwa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Wilaya Kilindi kwa asilimia 2.6. Mradi huo kwa sasa unatoa huduma chini usimamizi wa kamati ya maji ya Vijiji vya Kigwama na Muungano.

Naye Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo amesema tatizo hilo lingekuwa dogo kama Kamati za Maji za vijiji hivyo kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji zingekuwa makini kufuatilia ama kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wangeweza kulitatua.

“Mradi huu ulishakamilika na wananchi wakiwa wanapata maji. Lakini kuna maeneo ya viungio yalikuwa yameharibiwa na watu wasio waaminifu na kufanya maji safi kuchanganyika na maji ya mvua, na kufanya mabomba kutoa maji yasiyoridhisha.

“Lakini tuliweza kurekebisha, na sasa tatizo hilo limekwisha na wananchi wanapata maji safi. Na ili kujiridhisha, Mkuu wa Mkoa wa Tanga (Adam Malima) aliweza kufika na kuangalia mradi huo, na kuwauliza wananchi, na wao kukiri sasa maji yanayotoka ni safi na salama,” amesema Mhandisi Lugongo.