December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi wa maji Kilindi Asili kunufaisha wananchi 20,851

Na Yusuph Mussa,Timesmajira Online, Kilindi

WANANCHI 20,851wa vijiji vya Kilindi Asili na Kwamazuma, Kata ya Kilindi, Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga wanatarajia kunufaika na mradi mkubwa wa maji.

Mradi wa maji Kilindi Asili unatekelezwa na Serikali Kuu kwa fedha za Mfuko wa Maji wa Taifa (NWF) kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).

Hayo yamebainishwa17, 2023 na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kilindi Mhandisi Alex Odena wakati anasoma taarifa ya mradi huo kwa Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru kitaifa Abdallah Shaib Kaim aliyefika hapo kuweka Jiwe la Msingi.

Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru kitaifa Abdallah Shaib Kaim akikata utepe kabla ya kuweka Jiwe la Msingi mradi wa maji Kilindi Asili, Kata ya Kilindi, Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga.

Mhandisi amesema chanzo cha maji cha mradi huo ni kijito Msiri chenye uwezo wa kuzalisha lita 7,862,400 kwa siku, ambapo mahitaji ya watu kwa siku ni lita 1,217,600.

Mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi Scorpion Ltd, ambapo muda wa utekelezaji wake ni miezi sita, na mradi unatarajia kuhudumia vijiji viwili ambavyo ni Kilindi Asili na Kwamazuma.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Abdallah Shaib Kaim akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kilindi Alex Odena (kushoto) kwenye Mradi wa Maji Kilindi Asili, Kata ya Kilindi, Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Abel Busalama (kushoto).

“Ujenzi wa mradi huu umeanza kutekelezwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Januari 21, 2023 na unatarajia kukamilika Julai 21, 2023,utekelezaji wa mradi huu kwa ujumla umefikia asilimia 60, ikihusisha kazi za ujenzi wa banio la maji (intake) asilimia 95, ujenzi wa machujio ya maji asilimia 25, na ujenzi wa tenki la maji la lita 450,000 asilimia 65,”amesema Mhandisi Odena.

Mhandisi Odena amesema pia kuna ujenzi wa vituo 34 vya kuchotea maji asilimia 80, ununuzi wa bomba, uchimbaji mtaro ulazaji na uunganishaji wa mabomba ya mtandao wa kupeleka maji kwenye tenki na kusambaza kwenda kwa watumiaji wenye urefu wa kilomita 16.113, asilimia 20, na ujenzi wa Ofisi ya Usimamizi wa Mradi (CBWSO) asilimia tano.

Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo (kushoto) akiwa juu ya tenki ili kujiridhisha kabla ya Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru kitaifa Abdallah Shaib Kaim hajaweka Jiwe la Msingi Mradi wa Maji Kilindi Asili, Kata ya Kilindi, Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga.

Amesema, RUWASA kwa kushirikiana na jamii, wamepanda miti 750 ili kulinda chanzo hicho cha maji, lengo likiwa ni kupanda miti 5,000 kwa ajili ya kutunza mazingira na kulinda

Aidha amesema mradi huo umekadiriwa kugharimu kiasi cha zaidi ya bilioni 1.4 kati ya hizo zaidi ya milioni 988 ni ujenzi wa miundombinu na zaidi ya milioni 509 ni ununuzi wa bomba unaofanywa na RUWASA mpaka sasa mkandarasi amelipwa malipo ya awali zaidi ya milioni 149.

“Mradi huu utawezesha wananchi wapatao 20,851 kunufaika na huduma ya maji safi hivyo kuongezeka kwa idadi ya wananchi wanaopata huduma ya maji safi katika Wilaya ya Kilindi kwa asilimia 5.2 ya wakazi wote kwa mwaka wa fedha 2022/2023 utekelezaji wake bado unaendelea,”amesema Mhandisi Odena.