November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi wa kupeleka umeme wa Gridi Rukwa waanza

Upungufu wa umeme wazidi kupungua

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online,Dodoma

Katika jitihada za kuhakikisha maeneo yote nchini yanapata umeme wa uhakika, Serikali imeshaanza kutekeleza mradi wa kupeleka umeme wa Gridi katika Mkoa wa Rukwa kupitia mradi wa TAZA ulioanza kutekelezwa mwezi Novemba, 2023 na unatarajiwa kukamilika Mwezi Agosti, 2026.

Hayo yameelezwa leo bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga wakati akijibu swali la Mbunge wa Nkasi, Mhe. Aida Khenani aliyetaka kufahamu mkakati wa kumaliza changamoto ya upatikanaji umeme wilayani Nkasi Mkoa wa Rukwa.

Amesema kuwa, kwa sasa TANESCO inaendelea kufanya maboresho ya miundombinu ili kupunguza changamoto ya upatikanaji umeme mkoani humo na kujenga kituo kipya cha kupoza umeme.

Kuhusu hali ya upatikanaji umeme nchini amesema kuwa, upungufu wa umeme unaendelea kupungua akitaja takwimu kuwa, umepungua kutoka megawati 400 hadi 144 kwa siku ya leo.

Ameeleza kuwa, Serikali inaendelea kufanya juhudi mbalimbali ili kuboresha hali ya upatikanaji umeme nchini akitolea mfano utekelezaji wa Mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ambao inatarajiwa kuwa, katika mwezi wa Pili kuelekea Machi mwaka huu utaanza kuingiza megawati 235 katika Gridi ya Taifa.

Mhe. Kapinga pia amezungumzia kazi ya upelekaji umeme wa gridi mkoani Katavi ambapo ameeleza kuwa, tayari kuna mradi unaoendelea kutekelezwa na kwa sasa baadhi ya vituo vya kupoza umeme vimekamilika na hivyo, nguvu sasa inawekwa zaidi katika ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kwenda mkoani humo.