Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online
MRADI wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), umeelezwa kutokuwa na athari za kimazingira,kutokana na Serikali kuweka sera nzuri na teknolojia rafiki kwa mazingira, ili kulinda bayoanuai wakati wa upitishaji wa bomba hilo chini ya mto Zigi.
Hayo yameelezwa na Msimamizi wa mradi wa ujenzi wa bomba kuvuka mto Sigi,unaojumuisha ulazaji wa bomba na uchorongaji kwa ajili ya kuvusha bomba chini ya mto, Mhandisi Thomas Mhando, wakati akielezea maendeleo ya mradi kwenye eneo.

Amesema wakati wa utekelezaji wa shughuli za ujenzi wa bomba linalopita chini ya mto huo, suala la uhifadhi wa mazingira limepewa kipaumbele sambamba na kutoa elimu kwa wananchi juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji hasa cha mto Zigi.
Kwani mto huo ndio tegemeo kwa wananchi wa Tanga na mradi wa EACOP kwa ujumla,ambacho kinahudumia takribani watu 26,552 ambao wanapatiwa maji na Mamlaka ya Maji Tanga Uwasa.
Ameongeza kuwa,walikubaliana kuwawezesha pia wananchi wa vijiji saba vilivyoko karibu na maeneo ya utekelezaji wa mradi,kwa kuhakikisha wanapatiwa maji chini ya mradi wa makubaliano ambapo jumla ya bilioni 2.728 zilitolewa na EACOP kutekeleza mradi wa maji ili wananchi pia wapate maji.
Awali akizungumza kwenye eneo la utekelezaji wa mradi huo Mratibu wa kitaifa wa mradi kutoka TPDC,Asiadi Mrutu,amesema, kwa sasa uvushaji wa bomba kwenye mto Sigi unaendelea vizuri na umefikia asilimia 63 na unatarajiwa kukamilika Novemba, 2025.
Huku akiipongeza NEMC kwa kusimamia suala la mazingira kwenye mradi huo kwa kuhakikisha wanatembelea mara kwa mara ili kuona kazi inavyoendelea.

Kwa upande wake, Mhandisi kutoka kitengo cha Miradi Tanga Uwasa, Mhandisi Aaron Chanimbaga,ameishukuru EACOP kwa kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma ya maji saa 24 tofauti na ilivyokuwa awali, na bomba hilo lina uwezo wa kutoa lita za ujazo milioni 1.7,kwa siku na linahudumia wananchi wa Chongoleani, Ndaoya, Putini, Elani,Mleni, Mabokweni,na Kibafuti.


More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako