Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
SERIKALI imeahidi kusimamia kwa karibu zoezi la upembuzi yakinifu la Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP), ili kuhakikisha linafanyika kwa ufanisi unaotakiwa na kuleta matokeo chanya hasa katika sekta za Kilimo na Uvuvi na hivyo kuchagiza uchumi wa Buluu.
Akizungumza katia hafla fupi ya utiaji saini wa mikataba miwili ya Upembuzi Yakinifu wa ununuzi wa Meli za Uvuvi na ujenzi wa viwanda viwili vya kuchakata Samaki Kilwa na Fungurefu kupitia programu ya AFDP , Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amesema kusaini mikataba hiyo ni tukio la kihistoria litakalowezesha upatikani wa meli mbili za uvuvi wa Bahari Kuu na viwanda vya kuchakata mazao hasa ya samaki.
Aidha amesema hiyo ni Programu ya kimkakati inayolenga kuifanya Tanzania inakuwa moja katika nchi za Afrika na Afrika Mashariki ambayo inaongoza katika uchumi wa bahari.
Amewataka wahusika wote wa mradi huo kuhaikikisha wanausimamia kwa umakini ili kuleta matokeo yaliyotarajiwa.
Aidha amesema mkataba huo utatekelezwa kwa muda za siku zisizozidi 45 kwa gharama ya Shilingi milioni 348.
“Hii ni program ambayo Viongozi wakuu, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt.Hussein Ali Mwinyi, wanaifuatilia kwa karibu lengo ni kuimarisha uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa, pamoja na kuendeleza uchumi wa buluu.”amesema na kuongeza kuwa
“Kwa hiyo mkifanya kazi hii kwa weledi na kukamilisha kwa wakati uliopangwa mtakuwa mmeshiriki katika kutafisiri maono ya Viongozi wetu hawa wakuu,”
Kwa upande wake Mratibu wa programu hiyo Salimu Mwinjaka amesema kuwa programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP), ni ya miaka sita ambayo ilianza mwaka 2021/2022 hadi 2027/ 2028 na itagharimu jumla ya dola za Kimarekani milioni 77.4.
“Kati ya fedha hizi mkopo kutoka IFAD ni dola za Marekani milioni 58.8, serikali dola za Marekani milioni 7.8, sekta binafisi dola za Marekani milioni 8.5 na wananchi dola za Marekani milioni 2.4, ” amesema
Kwa muibu wa Mwinjaka , lengo la programu hiyo ni kuwa na uzalishaji endelevu wa kibiashara na wenye kuzingatia mazingira hususan uzalishaji wa mbegu za mazao ya Kilimo kama mahindi, alizeti maharage na mimea ya mikunde, uvuvi na ufugaji wa viumbe maji ambao unazingatia uwezeshaji wa akina mama na ushiriki wa vijana.
Amesema kuwa programu hiyo inatarajia kuwanufaisha watu trakibani milioni 1.3 zikiwemo kaya za Wakulima wadogo 200,000 ambao watakuwa wanapata mbegu bora za mahindi,alizeti na maharage.
“Upembuzi Yakinifu wa awali tayari umefanyika na kubainisha Meli hizo zitaleta tija kwa uchumi na kwamba katika Upembuzi Yakinifu huo umependekeza Meli ziwe na urefu wa mita 26 na kuingia mkataba na Kampuni ya Dar es Salaam Merchant Group (DMG).”amesema Mwinjaku
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi