January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mpogolo awaonya Wenyeviti serikali za mitaa kuchongesha mihuri

Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline,Dar

MKUU wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo, amewataka  wenyeviti wote  wa Serikali za mitaa wilayani humo kutochongesha mihuri na kutumika katika kuwahudumia wananchi, mpaka  Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam itakapotoa mwongozo.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema, halmashauri hiyo ya jiji ndiyo itakayo toa mihuri itakayotumika katika ofisi hizo na kusema kuwa endapo mwenyekiti yoyote wa Mtaa atabainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua kwani ni kinyume cha sheria.

Mpogolo ameyasema hayo leo Desemba 18, 2024 alipokuwa akifunga semina ya  kuwajengea uelewa wenyeviti  wapya  wa mitaa 159  ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Amesema, mihuri ni nyaraka ya Serikali  hivyo Serikali ndiyo yenye mamlaka ya kuiandaa na kuikabidhi  kwa watumishi wake kwaajili ya kuwahudumia wananchi.

“Ninawaomba  kama kuna waliochinga mihuri wairudishe au waifungie wasiitumie. Tupate mwongozo kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) , tupate mwongozo kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaa ambaye ataleta maelekezo,”ameeleza Mpogolo.

Pia amesema mihuri hiyo itaanza kutumiwa na wenyeviti wa serikali za mitaa mpaka pale watakapopewa miongozo na mamlaka husika na siyo vinginevyo.

Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wenyeviti hao kuendelea kuwahudumia wananchi kikamilifu na kuimarisha uhusiano.“Naomba  tusichomoke nje ya sheria, tuache matamanio tufuate maelekezo, kama kuna barua unaandika nenda kaiandike halafu mpelekee Afisa Mtendaji agonge muhuri,”alieleza.

Pia,amewakumbusha wenyeviti hao kuwa, barua zote wanazo idhinisha na kugonga mihuri nyingi zina kwenda katika Ofisi za Serikali hivyo wajihadhari  na matumizi ya mihuri iliyo kinyume na utaratibu.

“Tuvute subira muda siyo mrefu tutapata  maelekezo na tutaishi katika maelekezo, ni wajibu wangu kuwalinda nyie Msitamani kufanya jambo litakalo wapeleka katika kifungo,”ameeleza Mpogolo.

Sambamba na hayo, amewataka wenyeviti hao kusimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato ya Serikali, miradi  inayo tekelezwa katika maeneo yao na kuimarisha uhusiano wao na Serikali.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Charangwa Selemani,amewataka  wenyeviti hao,kuwa kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi na kutambua ni wakati gani wanakuwa upande wa wananchi na wakati gani kuwa upande wa Serikali.

Akizungumzia mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mustafa, Kata ya Pugu, Fikiri Rajabu ‘Timbwa’ amesema semina hiyo imewapa mwanga  wa uongozi na namna bora ya kuwatumikia wananchi.

“Tumepata semina ya siku tatu, juzi tulikutana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, kwa ngazi ya mkoa na jana tulianza semina ngazi ya wilaya na semina zimetupa maelekezo mazuri, tumejijenga kutumikia wananchi, kuwa rafiki  na kiungo muhimu  baina ya na Serikali na wananchi katika mitaa yetu,”amesema Timbwa.