Na. Israel Mwaisaka, TimesMajira Online, Rukwa
Shule Bora ni programu ya elimu inayolenga kuinua ubora wa elimu jumuishi inayotolewa kwenye mazingira salama ya kujifunzia kwa wasichana na wavulana kwenye shule za umma nchini Tanzania. Inafadhiliwa na Shirika la Misaada la Uingereza (UKAID) kutoka Serikali ya Uingereza.
Inatoa msaada kwenye mchakato wa utekelezaji wa Mpango wa Elimu wa Lipa Kulingana na Matokeo wa awamu ya pili (EPforR II) kitaifa.
Programu hii inafanya kazi katika mikoa tisa ya Tanzania bara kwa msaada wa kiufundi kutoka Cambridge Education kwa kushirikiana na ADD International, International Rescue Committee na Plan International wanatekeleza Programu hii katika Mikoa 9 ya Tanzania Bara ambapo Halmashauri 67 zenye jumla ya Shule 5,757 zinanufaika na programu hii. Mikoa hiyo ni Dodoma, Katavi, Kigoma, Mara, Pwani, Rukwa, Simiyu, Singida, na Tanga.
Thamani ya ufadhili ni Shilingi Bilioni 271 (Paundi milioni 89) kwa kipindi cha miaka 6 kuanzia mwaka 2021 hadi 2027. Programu inalenga kutekeleza vipaumbele vya Serikali vilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu –Education Sector Development Plan (ESDP).
Matokeo ya programu ya Shule Bora kwanza ni 1) Kujifunza,Wanafunzi wote wajifunze darasani, 2) Kufundisha: Kuimarisha nguvu kazi ya ufundishaji, 3) Ujumuishi. Wanafunzi wote wapo shule salama katika mazingira mazuri yanayoawezesha kumaliza shule ya Msingi na kuendelea shule ya sekondari na 4) Kuimarisha mifumo: Utoaji wa huduma za kielimu unaimarishwa ili kuthibitisha thamani ya fedha.
Mikoa Tisa (9) ya utekelezaji wa Mpango wa Shule Bora imechaguliwa na serikali ya Tanzania kuzingatia maeneo yenye ufaulu duni wa wasichana, ushiriki duni wa watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu na wenye uhitaji maalum, maeneo ya kijografia, molali duni ya walimu, ushiriki duni wa jamii.
Jumla ya Wanafunzi takribani 4,000,000 na Walimu 60,000 wanatarajiwa kufikiwa katika utekelezaji wa programu kati ya April 2022 hadi Machi 2027.
Mpango wa Shule Bora unaunga mkono jitihada za Serikali kuhimiza matumizi ya mbinu jumuishi shirikishi za ufundishaji na ujifunzaji, kuwabainisha na kuwa fanyia uchunguzi watoto wenye mahitaji maalumu. Pia Kutoa usaidizi kwa Serikali kwenye mipango yake ya Ki-Elimu na mahitaji ya vituo vinavyotoa usaidizi kwa watoto wenye ualbino na uoni hafifu.
Aidha Mpango huu utatoa vifaa saidizi vya kufundisha Kusoma, Kuandika na Kuhesabu kwa Watoto wenye tatizo la kuona na kusikia ikiwa na sambamba na kutoa mafunzo kwa watoto wenye tatizo la mtindio wa ubongo (autism).
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Maendeleo toka Ofisi ya Ubalozi wa Uingereza nchini Mama Kemi Williams wakati wa mazungumzo na Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Bwana Rashid Mchatta (Februari 01,2023) mjini Sumbawanga.
Mradi wa Shule Bora unalenga kuweka mikakati sahihi na kutafuta suluhisho ili kuhakikisha watoto wote wakiwemo wenye ulemavu,wanaoishi katika mazingira magumu, wasichana na wavulana wanapata elimu bora ya Msingi na kuendelea na Elimu ya Sekondari.
Kemi pamoja na Mshauri wa Elimu Ubalozi wa Uingereza Ndugu John Lusungu walifanya ziara ya siku mbili mkoani Rukwa 1-2/02/2023 ambapo walitembelea shule za msingi Kinamwanga na Kizwite zilizopo Manispaa ya Sumbawanga na kukutana na kuzungumza na walimu wakuu, walimu, wawakilishi wa wazazi, Maafisa elimu Kata na kamati za shule kujifunza namna wanavyosimamia utoaji elimu ya msingi mkoani.
Viongozi hao wa Ubalozi wa Uingereza wakishirikiana na Viongozi wa elimu Mkoa na Halmashauri za Wilaya Sumbawanga na Manispaa ya Sumbawanga walishiriki upandaji wa miti 12 (6 ya matunda na 6 ya vivuli) ya kumbukumbu ya Ushirikiano wa Serikali ya Watu wa Uingereza na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiwa ziarani Shule ya Msingi Kizwite, mjini Sumbawanga.
Mama Kemi alisema ‘Nimekuja kujifunza na kujionea uhalisia wa utolewaji elimu ngazi ya msingi kwa kuona na kuzungumza na walimu na wazazi. Nimefarijika kuona Nkasi na Kalambo kuna hatua za kuwaunganisha watoto waliokuwa nje ya mfumo rasmi wa elimu kupitia vituo vya utayari chini ya mradi wa Shule Bora” alisema Kemi.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa, Ndugu Rashid Mchatta alisema anaipongeza serikali ya Uingereza pamoja na washirika wake kwa kutoa ufadhili kutekeleza mradi wa shule bora ambapo mkoa wa Rukwa, shule za Serikali 382 za Msingi zinanufaika na mpango huu.
“Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa Mikoa 9 ya utekelezaji wa Mpango wa Shule Bora iliyochaguliwa na serikali ya Tanzania kuzingatia maeneo yenye ufaulu duni wa wasichana, ushiriki duni wa watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu na wenye uhitaji maalum, ukizingatia maeneo magumu kufikika kijografia aidha molali duni ya wazazi kushiriki katika maendeleo ya kielimu pia molali duni miongoni mwa walimu katika ufundishaji” alisema Mchatta wakati wa mazungumzo na mwakilishi wa Ubalozi wa Uingereza.
Ndugu Mchatta aliongeza kusema serikali itatoa ushirikiano ili mradi wa Shule Bora katika miaka yake sita ya utekelezaji uweze kufanikiwa na watoto wengi hususus waliopo mazingira magumu na wasichana wapate fursa ya kusoma elimu ya msingi.
Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana tangu kuanza kwa mradi, Mratibu wa Shule Bora Rukwa Bwana John Shindika alisema kupitia programu ya utayari kuanza shule kwa 2022 iliyoendeshwa katika vituo 17 katika halmashauri 4. Mafunzo ya Watoto walio nje ya mfumo wa utayari wa kuanza shule ya wiki 12 yamefanyika mwezi Oktoba hadi Disemba 2022 ambapo Watoto 2,640 (wavulana 1,350 na wasichana 1,290) wamenufaika na mafunzo hayo katika vituo 17 vya utayari wa kuanza shule toka Shule Mama za Msingi 16 ndani ya Kata 8 zilizoteuliwa kwa mwaka 2023.
Mradi umewezesha Watoto 2,242 waliokuwa nje ya mfumo rasmi wa madarasa ya awali kwa mwaka 2022 kuweza kuanza shule mwaka 2023 ambapo watoto 1,341 (wav 705 na was 636) wameandikishwa darasa la Kwanza. Pia Watoto 680 (wav 392 na was 288) wameandikishwa kuanza madarasa ya awali huu, aidha Watoto walioandikishwa MEMKWA ni 221 (wav 120 na was 101) kadhalika watoto 11 (wav 6 na was 5) wenye mahitaji maalum wameandikishwa kuanza shule 2023 kwa shule Mama 16 zilizokuwa na vituo 17 vya utayari wa kuanza shule Mkoani Rukwa.
Hata Hivyo Shindika aliongeza kusema idadi ya Watoto wote waliaondikishwa katika Shule Mama za Msingi 16 zilizoteuliwa kuwa kuendesha Vituo 17 vya utayari wa Watoto 3,392 (wav 1,641 na was 1,751) wameanza shule na wanaendelea na masomo darasani kwa mwaka 2023, Idadi hiyo ni kwa shule zilizoendesha vituo vya utayari wa kuanza shule.
Naye mkazi wa kijiji cha Kinamwanga Manispaa ya Sumbawanga Bwana Anyitile Mwezimpya aliiomba serikali kuboresha madarasa yaliyopo klwa kujenga zaidi ili shule ya msingi Kinamwanga watoto wasome vizuri pamoja na kuongeza walimu kwani kwa sasa ina walimu nane na wanafunzi 381 huku kukiwa hakuna mwalimu wa darasa la awali na la kwanza.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika