November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mpango wa matumizi bora ya ardhi kumaliza changamoto ya migogoro ya ardhi vijijini.

Na Suleiman Abeid,Timesmajira Online,Shinyanga

CHANGAMOTO ya migogoro ya ardhi ikiwemo ugomvi wa kugombania maeneo ya mipaka kati ya kijiji na kijiji wilayani Kishapu mkoani Shinyanga hatimaye imepatiwa ufumbuzi baada ya serikali kuanza kutekeleza mpango wa taifa wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji 16 vilivyopo wilayani humo.

Utekelezaji wa mpango huo unakwenda sambamba na uwekaji wa vigingi (bicons) zinazotambuliwa kisheria hii ni baada ya kukamilika kwa zoezi la urasimishaji maeneo mbalimbali ya vijiji ambapo mikutano mikuu ya wanakijiji imefanyika na kupitisha urasimishaji huo baada ya kazi iliyofanywa na Kamati za Usimamizi ardhi za vijiji.

Mmoja wa wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya matumizi ya ardhi akifafanua jambo kwa wanavijiji vya Mwigumbi na Buganika kabla ya kuanza kwa zoezi la uwekaji bicons kwenye mipaka ya vijiji vyao.

Baadhi ya wananchi ambao wameshiriki kwenye zoezi la uwekaji vigingi katika mipaka ya vijiji vya Mwigumbi, Buganika,Buchambi na Songwa wilayani Kishapu wameelezea kufurahishwa na hatua hiyo ya serikali ambayo wamesema itamaliza kabisa ugomvi wa kugombania ardhi katika vijiji vyao.

Wamesema kwa kipindi kirefu kumekuwa pakijitokeza migogoro ya mara kwa mara ya kugombania maeneo ya ardhi kati ya wanakijiji kwa wanakijiji lakini hata upande wa kijiji na kijiji vikigombea maeneo ya mipaka kutokana na kutokuwepo na mipaka inayotambulika kisheria.

Kwa upande wao baadhi ya wanakijiji akiwemo Yusufu Bala mkazi wa kijiji cha Songwa wilayani Kishapu amesema hatua ya serikali kutekeleza mipango ya matumizi bora ya ardhi inastahili kupongezwa na wapenda amani wote.

Amesema kwa kipindi kirefu pamekuwa na migogoro ya kugombania ardhi katika maeneo mengi vijijini kutokana na kutokuwa na alama za kudumu zinazotenganisha maeneo ya ardhi kati ya mtu na mtu na hata mipaka ya kijiji na kijiji.

“Hili zoezi linaloendelea ni zoezi tunalolifurahia isipokuwa lilikuwa limechelewa, lakini kwa sasa tumepata uhakika wa umiliki wa maeneo yetu baada ya vijiji vyetu kupimwa, hata ile migogoro ya kijiji na kijiji kugombania mipaka sasa haitokuwepo tena, tunaishukuru serikali yetu,” ameeleza Yusufu.

Wakazi wa vijiji vya Mwigumbi na Buganika wilayani Kishapu mkoani Shinyanga wakishuhudia uwekaji wa moja ya bicons katika mpaka unaotenganisha kijiji cha Mwigumbi na Buganika.

Naye mkazi wa kitongoji cha Buganika Kata ya Mondo, Zengo Mipawa amesema upimaji wa vijiji kupitia mpango wa taifa wa matumizi bora ya ardhi utapunguza migogoro na hata vifo na kwamba utaratibu huo umefanyika kwa kuwashirikisha watu wengi na kila mtu ameridhia.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mondo wilayani Kishapu, Ndotto Matata ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia kwa kuhimiza suala la vijiji kupitisha mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji vyao.

Matata ametoa angalizo kwa wanavijiji wote ambako utaratibu wa uwekaji wa mipaka umefanyika wajitahidi kuvitunza vigingi vilivyowekwa ambavyo vimezingatia sheria za nchi na kwamba mtu yeyote atakayeharibu au kuving’oa kwa makusudi atapambana na mkono wa sheria.

Kwa upande wake Ofisa Mipango Miji na Vijiji kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya matumizi ya Ardhi makao makuu Dodoma, Fadhili Makame amesema lengo la serikali kuendesha zoezi hilo ni kuweza kurathimisha maeneo ya ardhi ya vijiji na kuviwekea mpango bora wa matumizi yake.

Amesema katika vijiji 16 vya Wilaya ya Kishapu vilivyoteuliwa kuendesha mpango huo wananchi wamepata fursa ya kupatiwa elimu juu kuuelewa mpango wa matumizi bora ya ardhi na wanakijiji wakachagua kamati zao za usimamizi wa ardhi katika vijiji vyao.

Amesema katika zoezi hilo wanakijiji wametenga matumizi ya ardhi kwa kuteua maeneo kwa ajili ya kilimo, makazi, malisho ya mifugo, ujenzi wa nyumba za taasisi mbalimbali ikiwemo shule na maeneo ya makaburi na kwamba kamati za usimamizi pia zimeandaa sheria ndogo za kulinda matumizi hayo.

“Mipango hii itawawezesha wananchi kunufaika na ardhi zao iwapo watapima na kupatiwa hatimiliki za kimila ambazo zitaongeza thamani ya ardhi wanazozimilika,pia zoezi hili linaenda sambamba na kujua maeneo ya mipaka kati ya kijiji na kijiji,”amessma na kuongeza kuwa

“Zoezi hili linalofanyika hapa katika kata ya Mondo na Songwa limelenga kuondoa changamoto ya kijiji kimoja kupanga mipango yake ya matumizi ya ardhi na kutoka nje ya kijiji husika na kuingia kijiji kingine, hivyo tumekutanisha pande zote mbili na wamekubaliana na tukaweza kuweka bicons katika mipaka yao,” ameeleza Makame.