November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Meneja wa uthibiti ubora kiwanda cha viwadudu Kibaha Mkoani Pwani, Samweli Mziray.

Mpango wa kutokomeza malaria wazinduliwa jijini Mbeya

Na Esther Macha,Timesmajira, Online, Mbeya

MPANGO wa Kitaifa wa kutokomeza ugonjwa wa malaria nchini kwa kuangamiza viluwiluwi vya mbu waenezao ugonjwa huo umezinduliwa mkoani Mbeya.

Mpango huo utaanza kutekelezwa katika Mikoa ya Mbeya na Songwe kabla ya kusambaa nchi nzima.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Meneja Ubora wa Kiwanda cha Viuadudu kilichopo Kibaha mkoani Pwani, Samweli Mziray, amesema mpango huo unalenga kutokomeza malaria nchini ifikapo mwaka 2025 .

Mziray amesema mpango huo unatekelezwa kwa kuangamiza viluwiluwi vya mbu kwa kutumia dawa ya kuua wadudu inayozalishwa kutoka kwenye kiwanda cha Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) .

Mratibu wa mpango huo, Jackson Cyprian alidai kiwanda hicho ni cha pekee kinachozalisha dawa hiyo barani Afrika.

“Tuna sababu za kujivunia uwepo wa kiwanda kwa Afrika ambacho tunaamini kuwa kitaweza kusaidia kuinua mpango wa kutokomeza ugonjwa malaria nchini,“amesema mratibu huyo.

Akizindua Mpango huo mkoani Mbeya, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, ameziagiza Halmashauri zote za mkoa huo kutenga bajeti ya ya kununua dawa hiyo ili kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa ufanisi.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Dkt. Jonas Lulandala amesema maambukizi ya malaria mkoani Mbeya ni asilimia tatu na kwamba mpango huo utasaidia wananchi na wageni wanaoingia mkoani humo kutougua malaria.