Na Jackline Martin, TimesMajira Online
SERIKALI imekusudia kuja na mpango na usimamizi endelevu wa matumizi ya Rasilimali za Bahari ikiwa ni pamoja na mgawanyo sahihi wa matumizi ya bahari ikiwa ni pamoja na kuweka mipaka kwaajili ya sekta ya uvuvi mafuta na usafirishaji.
Hayo ameyasema Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mary Maganga wakati akifungua warsha ya mafunzo ya kikanda kuhusu mpango wa matumizi ya sekta ya bahari (Marine Spatial Planning -MSP) na ukanda wa Pwani ya Magharibi mwa Bahari ya Hindi hapo leo jijini Dar es Salaam.
Lengo ni kuwajengea uwezo wataalamu kutoka nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi, kubadilishana uzoefu na kufahamu hatua zilizofikiwa na nchi wanachama katika kuandaa na kutekeleza mpango huo.
“Ninapozungumzia uchumi wa bluu ninasisitiza usimamizi endelevu na shirikishi wa mifumo ikolojia ya Pwani na bahari ya Tanzania ili kuendelea kutoa bidhaa na huduma muhimu ikiwa ni pamoja masuala ya uvuvi na uchimbaji wa mafuta na gesi pale vitakakapogundulika,” alisema.
Aidha, Maganga amesema Tanzania ni mwenyeji wa kikao kazi hicho kinachohusisha wajumbe kutoka zaidi ya nchi 10 wanaotekeleza Mkataba wa Nairobi unaohusu Hifadhi, usimamizi na uendelezaji wa Mazingira ya Bahari na Ukanda wa Pwani ya Magharibi.
“Warsha hii imehusisha nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi na nchi zinazoshiriki ni pamoja na Tanzania, Komoro, Kenya, Somalia, Madagascar, Mauritius, Msumbiji, Shelisheli, Re-Union na Afrika Kusini,”alisema Maganga.
Amesema baada ya mafunzo hayo watakuwa wamejifunza namna bora ya kugawa rasilimali hizo za mahali na takwimu ambazo zinatokana na viumbe hai ambavyo vimo humo.”Kwa wenzetu wa Zanzibar kuna uoto mwingi wa asili na kwetu Bara unaonekana kandokando ya bahari na lakini pia tunautunza vipi na mazingira yake yawe endelevu tunafanya namna gani”
Kwa upande wa wavuvi, Maganga amesema ni muhimu kujua mipaka yao na kujua ni wapi ukomo wa kufanya biashara hiyo.
Naye Meneja wa Tafiti za Mazingira kutoka NEMC, Rose Mtui amesema mkutano huo ni muhimu kwa kanda na kwa nchi kwa ujumla, kwani utawasaidia sana kama nchi inapoingia kwenye uchumi wa buluu.
Dkt. Siajari Pamba, ambaye ni Mhadhiri na Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Kua na teknolojia ya uvuvi kutoka Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam amesema warsha hiyo ya mafunzo ni muhimu kwao kwani wamepata fursa ya kushirikishana kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Afrika Kusini ambao wameshapiga hatua zaidi kwenye mpangilio wa Masuala ya matumizi ya bahari.
More Stories
Balozi Nchimbi kuongoza waombolezaji mazishi ya Kibiti leo
Dkt.Tulia,apewa tano kuwezesha wananchi
Nkasi yajipanga kukusanya mapato