May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mpango Kabambe wa Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia ulivyoanza kwa kasi

Na Athuman Abdallah,Timesmajiraonline, Iringa

WIKI hii Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, amezindua Mpango Kabambe wa Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia unaolenga kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.

Kupitia mpango huo madaktari hao watakuwa wanatoa huduma za kibingwa katika hospitali zote za halmashauri 184 nchini kote.

Dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za afya.

Kupitia uzinduzi wa mpango huo, dhamira hiyo ya Rais Samia imepata msukumo mpya baada ya kuzinduliwa Mpango Kabambe wa Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia katika hospitali za halmashauri za wilaya nchini.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Waziri Ummy Mpango wa Dkt Samia wa kusogeza zaidi karibu na wananchi huduma za madaktari bingwa ambao kauli mbiu zao ni Madaktari Bingwa wa Dkt Samia, tumekufikia karibu tukuhudumie.

Amesema Mpango huu utafika katika Halmashauri zote 184. Alisema Serikali imeangalia huduma zenye uhitaji zaidi.

Kwa mujibu wa Waziri Ummy, timu ina madaktari bingwa 25, madaktari bingwa wa afya ya uzazi na wanawake, watoto na watoto wachanga, daktari bingwa wa upasuaji, daktari bingwa wa magonjwa ya ndani, daktari bingwa wa usingizi na ganzi. Wote watafanya kazi za kibingwa kwa siku tano kwa hospitali za mkoani Iringa.

Amesema Mei 13 hadi 17 watakuwa na madaktari bingwa 190 katika hospitali 38 za Kanda ya Kati na Nyanda za Juu Kusini Magharibi, Mikoa ya Dodoma, Singida, Manyara, Rukwa, Songwe na Mbeya.

Mei 20 hadi 24 Madaktari Bingwa wa Rais Samia watakuwa katika Mikoa 3 ambayo ni Dar es Salaam, Pwani na Morogoro itakayojumuisha madaktari bingwa 120 na kutoka huduma katika hospitali za halmashauri.

Mpango huu utaendelea katika hospitali zote ili kupunguza vifo na kupunguza pia mateso ya wagonjwa haswa wale wanaoshindwa kwenda kwenye hospitali za rufaa.

Serikali imejenga majengo ya kisasa pamoja na uwekezaji kwenye vifaa tiba. Mashine ya CT Scan kwa sasa inapatikana katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa. Hata kwenye Hosptal ya Wilaya ipo mashine ya kisasa ya digital x-ray.

“Zamani watu wenye changamoto za kuugua figo ilikuwa lazima waende Dar es Salaam, lakini leo Serikali imewekeza sana kuongeza wataalam wa afya,” amesema Ummy.

Amesisitiza ubora wa huduma, kujengeana uwezo na kubadilishana uzoefu. “Rais Samia ameandika rekodi duniani na barani Afrika ya kupunguza vifo vya akina mama wajawazito kwa asilimia 80.

Kutoka vifo 556 katika kila viazi laki moja hadi vifo 104 katika kila vizazi hai 100.

“Tumsaidie Rais Samia aandike rekodi nyingine duniani ya kupunguza vifo vya watoto vya wachanga kwa sababu hatujafanya vizuri. Vifo vya watoto wachanga vimepungua kwa asilimia 4 tu.

Kutoka vifo 25 katika kila vizazi hai 1000 hadi vifo 24 katika vizazi 1000. Tukiwekeza vizuri kwenye wodi za watoto wachanga tutapunguza vifo vya watoto wachanga hadi asilimia 50,” alisema Ummy.

“Shirika la Afya Duniani linaeleza kwamba tukiwekeza kwenye wodi za watoto wachanga tutapunguza vifo vya watoto wachanga kwa zaidi ya asilimia 50, ndiyo maana tumeanzisha mpango huu kabambe wa madaktari bingwa wa Dkt. Samia ili kuweka msukumu wa kuanzishwa kwa wodi za watoto wachanga ili kuokoa maisha ya watoto wachanga katika hospitali za halmashauri za nchini.

Alisema jambo hilo, sio jambo gumu, linahitaji utashi wa kisiasa, linahitaji usimamizi wa viongozi wote katika ngazi ya mikoa na wilaya.

Amesema wao kama Serikali watanunua vifaa, lakini anatamani vifaa hivyo vipelekwe kwenye ngazi ya vituo vya afya hospitali ya halmashauri hizo kidogo zina mapato.

Mara baada ya uzinduzi huo, tayari madaktari bigwa wameanza kusambaa maeneo mbalimbali nchi kutoa huduma za kibingwa, tofauti na zamani, ambapo wananchi iliwalazimu kusafiri kwenda Dar es Sakaam kufuata huduma hizo.

Mfano, wiki hii timu ya madaktari bigwa 30 imefika katika Hospitali ya Mji wa Njombe Kibena na kushuhudia huduma za kibingwa zikiendelea.

Mwandishi wa makala haya alishuhudia mama mjamzito aliyefanyiwa upasuaji chini ya uangalizi wa madaktari hao.

Dkt. Erenestina Mwipopo, ambaye Daktari Bingwa Mbobezi wa magonjwa ya watoto anasema tayari ameanza kuwahudumia watoto na baadhi ya aliowahudumia ni wenye magonjwa ya moyo, waliozaliwa kabla ya wakati pamoja na wenye changamoto nyingine.

“Hapa Njombe mjini tupo madaktari bingwa watano na tumegawanyika kwenye idara tofauti, lakini hapa kwenye watoto wachanga tumeshaanza kuwahudumia pia na kuna mtoto mwenye changamoto ya moyo anapatiwa huduma na upande wa akina mama tayari upasuaji umeanza,”anasema Dkt. Mwipopo

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji wa Njombe Kibena, Dkt. Ayub Mtulo amesema wagonjwa wameendelea kujitokeza katika hospitali hiyo ambapo wengi wao wamekuwa wakifika kwa dakatari bingwa wa wanawake na uzazi.

“Wanaofika kwa wingi ni wateja wa daktari bingwa wa wanawake pamoja na uzazi pamoja na magonjwa ya ndani, lakini pia daktari bingwa wa upasuaji amepata wateja,”anasema.

Timu hiyo ya madaktari bingwa ni miongoni mwa madaktari bingwa katika mpango kabambe wa utoaji huduma za kibingwa kwenye hospitali 184 katika ngazi ya halmashauri zinazofanywa na madaktari bingwa wabobezi wa Dkt. Samia

Lakini pia ameongeza juhudi za kuhakikisha taifa letu linakuwa na madaktari bingwa wa kutosha kupitia Dkt. Samia Super-Specialized scholarship Programme.

Kupingia mpango huo, tayari Serikali ya Rais Samia imetoa nafasi za ufadhili wa masomo ya ubingwa na ubingwa bobezi, ambapo kwa mwaka wa masomo 2023/2024, jumla ya sh. 10.9 bilioni zimetengwa na kuwawezesha wanafunzi 1,109 kwenye masomo ya ubingwa na ubingwa bobezi.

Takwimu hizo zimetolewa na Waziri Ummy Mei 2, 2024 wakati akifungua mkutano wa Mwaka wa Chama cha Madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani Tanzania (APHYTA) uliofanyika katika ukumbi wa Kinataifa wa Mwalim Julius Nyerere Jijini Dar Es Salaam.

“Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa madaktari bingwa katika kuwaendeleza kitaaluma kupitia programu ambayo imetoa nafasi za ufadhili wa masomo ya ubingwa kwa mwaka wa masomo 2023/2024, kwa wanafunzi 1,109 ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 582 ukilinganisha na mwaka wa masomo 2022/2023.” Anasema Waziri Ummy

Anasema katika idadi ya wanafunzi wote ambao wamepata ufadhili kupitia programu hiyo, wanafunzi 79 watasomea udaktari bingwa wa magonjwa ya ndani na kati yao madaktari 11 sawa na asilimia 33 wamekwenda kusoma ubingwa bobezi wa magonjwa ya ndani.

Aidha, Waziri Ummy ametoa wito kwa madaktari vijana kujitokeza kwa wingi kwenda kujiendeleza katika masomo ya ubingwa bobezi hususan kwenye magonjwa ya ndani na wakirudi wakubali kupangiwa sehemu yoyote kwa kuwa mikoa mingine pia inahitaji madaktari bingwa bozezi.

“Kupitia muundo huu mpya wa Sekta ya Afya, tutaweza kuwatambua kwa kuwawekea mazingira mazuri madaktari wenye Ubobezi katika maeneo mbalimbali ikiwemo wa masuala ya magonjwa ya ndani.” Amesema Waziri Ummy

Katika hatua nyingine Waziri Ummy amewataka madaktari hao kujadiliana na kuja na mapendekezo ya jinsi ya kupunguza magonjwa Yasiyoambukiza kwa kuwa kwa sasa kumekuana ongezeko kubwa la magonjwa hayo.

Pia, Waziri Ummy amewataka madaktari hao kujadiliana na kutoa maoni yao katika muongozo wa Kitaifa wa matibabu pamoja na orodha ya Taifa ya dawa ili kama kuna mapungufu yaweze kurekebishwa.