Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Arusha
MAKAMU wa Rais wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amezitaka taasisi za fedha hususan benki, kupunguza riba kwa wakopaji ili mikopo wanayokopa iweze kuwaletea ufanisi kwenye shughuli zao.
Lakini pia ametaka juhudi za makusudi zifanyike ili kuwashawishi wananchi kununua hisa kwenye benki na kampuni nchini, ambapo hisa hizo zitawasaidia kupata faida na kuendesha shughuli zao za kila siku.
Aliyasema hayo Mei 19, 2023 wakati anafungua semina iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa Wanahisa wake kuelekea Mkutano Mkuu wa 28 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB utakaofanyika Mei 20, 2023 kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa kwenye Ukumbi wa Simba jijini Arusha.
“Nitoe wito kwa wenye mabenki na taasisi nyingine za kifedha, muweze kupunguza riba kwa watu wanaokopa, na ikiwezekana iwe chini ya asilimia tisa. Hiyo itawasaidia wakopaji kuweza kunufaika na mikopo hiyo na kuweza kufanya shughuli zao, na kupata faida.
“Pia nakubaliana na Mwenyekiti (Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB Dkt. Ally Laay), kuwa suala la hisa lifundishwe kama Mtaala shuleni, na nadhani Waziri wa Elimu (Profesa Adolf Mkenda) yupo hapa, na amesikia. Ni kweli, wananchi waliopo kwenye Soko la Hisa ni wachache sana” alisema Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango alisema, bado huduma za kibenki ni chache kwa maeneo ya vijijini, na ni asilimia 8.6 ya wananchi wa vijijini wanapata huduma za kibenki, hivyo imefika wakati kwa benki nchini kuongeza wigo wa kutoa huduma za kifedha maeneo ya vijijini.
Aliwapongeza Benki ya CRDB kwa kuanzisha Taasisi ya CRDB Bank Foundation ambayo inashughulika kutoa mikopo kwa vijana na wanawake, nakusema huko sasa ndiyo kuna uwanja mpana kwa watu kukopa na kufanya shughuli zao za ujasiriamali.
“Ndugu Wanahisa na wageni waalikwa,
napenda kutumia fursa hii pia kuwapongeza Benki ya CRDB, kupitia kwa taasisi yenu ya CRDB Bank Foundation kwa ubunifu wenu wenye manufaa makubwa na tija kwa Taifa kupitia programu ya ”iMBEJU” ambayo ilizinduliwa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), katika semina yenu ya Uwekezaji. Nimefurahia msisitizo mlioweka kukuza biashara changa na kwa kuwaalika vijana wenye biashara changa za kibunifu “start-ups” pamoja na wanawake katika semina hii.
“Napenda pia kuzipongeza start-ups nilizozitembelea, kwani nimeona ubunifu mkubwa sana kwa vijana wetu. Changamoto tuliyonayo kama Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta binafsi kama Benki ya CRDB, ni kuhakikisha start-ups hizi haziishii njiani bali zinafikia hatua ya kuwa biashara kubwa ambazo zitakua na manufaa makubwa kwa wabunifu wetu, lakini na Taifa kwa ujumla kupitia ajira, mapato na kodi mbalimbali za biashara” alisema Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango pia ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuvuka mipaka ya nchi na kwenda kuanzisha huduma za kibenki kwenye nchi za Burundi, na sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
“Pia nawapongeza kwa kuongeza mawanda (wigo) kwa kuanzisha Benki ya CRDB Burundi (sasa miaka 10), na sasa mnakwenda kuanza nchi ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo (DRC), hayo ni mafanikio makubwa kwa benki” alisema Makamu wa Rais.
Makamu wa Rais alisema, Serikali ya Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka mazingira mazuri ya kufanya biashara, uwekezaji na ujasiriamali, na itaendelea kufanya hivyo siku zijazo, kwani ina nia ya kuwainua kiuchumi, mwananchi mmoja mmoja, na Taifa kwa ujumla.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB Dkt. Ally Laay alisema, pamoja na Watanzania kufikia milioni 61.7, bado wapo kidogo kwenye Soko la Hisa, hivyo kuwepo mkakatii ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa Mtaala shuleni utakaofundisha mambo ya fedha ikiwemo uwekezaji wa hisa.
“Watanzania tupo wengi, lakini waliopo kwenye Soko la Hisa ni kidogo sana. Hivyo, kuwe na Mtaala tangu shuleni utakaoelezea mambo ya hisa, shughuli za fedha na uwekezaji kwenye masuala ya kiuchumi. Soko la Hisa lina faida kubwa kuliko kilimo, ufugaji na uvuvi” alisema Dkt. Laay.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Group Abdulmajid Nsekela, alijinasibu kuwa wao ndiyo benki ya kwanza kuanzisha rasmi Huduma ya Bima nchini, lakini benki ya kwanza kuweza kuwa na huduma za kibenki nje ya nchi, na pia kuwa ya kwanza kuanzisha Taasisi ya CRDB Bank Foundation ambayo inakwenda kuwapa mitaji ya uwezeshaji vijana na wanawake.
Nsekela alisema, Benki ya CRDB imekuwa ikiimarika kila mwaka kwa kuongeza faida na thamani ya hisa zake, ambapo kwa mwaka 2022, baada ya kodi, imeweza kupata faida ya sh. bilioni 351 ikilinganishwa na sh. bilioni 36 kwa mwaka 2017, na hilo ni ongezeko la asilimia 875.
Na kutokana na ukuaji huo wa faida, thamani ya hisa imepanda sokoni, ambapo baada ya CRDB kutangaza matokeo yao ya hesabu za fedha hivi karibuni, hisa imepanda hadi sh. 510, ambapo mwaka 2017 bei ya hisa moja ya Benki ya CRDB ilikuwa sh. 90, na hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 567 ndani ya miaka mitano.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja