January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mpango ateta na Makamu wa Rais Benki ya Dunia

Na Mwandishi wetu,timesmajira,Online

Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango hii leo Septamba 28, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Dkt Hafez Ghanem Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais Dkt. Mpango amemuhakikishia Dkt. Ghanem kwamba Tanzania itaendelea kushirikiana na Benki hiyo katika masuala mbalimbali ya kuinua uchumi hapa nchini.

Makamu wa Rais Dkt. Mpango amesema kwamba serikali ya awamu ya sita imeweka kipaumbele katika kuinua sekta binafsi pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji hapa nchini. Amesema mpango wa maendeleo wa miaka mitano umelenga kuinua sekta ya viwanda hapa nchini hivyo serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kufanikisha hilo.

Aidha Makamu wa Rais Dkt. Mpango amesema ili kukidhi mahitaji ya sekta binafsi hapa nchini serikali imeweka mkazo katika sekta ya elimu hasa elimu ya ufundi ili kupata wahitimu wenye ujuzi watakaoweza kusaidia kuinua sekta hiyo.

Makamu wa Rais amesema serikali ya awamu ya sita imeendelea kuimarisha utawala bora pamoja na kudhibiti rushwa hapa nchini hivyo kuweka mazingira rafiki ya kutekeleza miradi mbalimbali.

Kwa upande wake makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Hafez Ghanem amesema Benki ya Dunia itaendelea kuiunga mkono Tanzania katika masuala mbalimbali
huku akitaja maeneo ambayo benki hiyo itashirikiana na Tanzania kwa sasa ambayo ni pamoja na uboreshaji miundombinu ikiwemo ya Nishati na Tehama, mapambano dhidi ya uviko19 pamoja na kuinua uchumi baada ya janga la Uviko 19.