November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu Mkuu Bashiru Ally akimkaribisha Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli katika kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa kilichoketi leo tarehe 9 Julai 2020 Jijini Dodoma. Picha na CCM

Moshi mweupe Urais Zanzibar wafukuta

Kamati Kuu yahitimisha, kuwasilisha mapendekezo NEC leo, wagombea watakiwa kuwa wanyenyekevu taarifa zao zinapojadiliwa

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma

KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi imekutana jijini Dodoma na kufanyia kazi taarifa ya Kamati Kuu Maalum ya Visiwani Zanzibar, kupokea taarifa kutoka Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na taarifa ya Kamati ya Usalama wa Maadili ya CCM Taifa kuhusiana na makada wa Chama hicho wanaoomba kusimamishwa kuwania Urais Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, amesema kikao hicho kimejadili kwa kina taarifa hizo, kimefikia uamuzi ambao utawasilishwa leo kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho.

Amesema kikao hicho kimefanya uamuzi kwa maslahi mapana ya Taifa la Tanzania na Zanzibar.

“Uamuzi wa kikao hicho utawasilishwa kesho (leo) kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ambayo ndio yenye dhamana ya kupigia kura mapendekezo ambayo yametafakariwa na kupelekwa na Kamati Kuu kwenda kwenye Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM,” amesema Polepole.

Amesema kikao hicho cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kimefanyika chini ya Mwenyekiti wake, Rais John Magufuli na imeketi na imefanyia kazi mazingatio yote ya kikatiba na kikanuni.

Amesema mapendekezo ya wanachama wa chama hicho ya kuomba ridhaa ya kupeperusha Bendera ya CCM kwa nafasi ya urais Zanzibar na Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yatajadiliwa leo.

Ametumia fursa hiyo kuwataka wagombea kuwa watulivu na unyenyekevu katika kipindi hiki ambacho taarifa zao bado zinajadiliwa .

“Tunawataka wote walioshiriki kuwania nafasi hiyo waendelee kuwa wanyenyekevu taarifa zote zinajadiliwa na kesho (leo) zinapelekwa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ambacho ndio chenye dhamana ya kufanya uchaguzi wa majina kwa Rais wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema.

Aidha amesema Mkutano Mkuu utakaofanyika Julai 11 na 12 ndio utahitimisha kwa kuwataja wagombea wa urais watakaopeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.