Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
KANISA la Moravian usharika wa Nyakato umezindua studio kwa ajili ya kurekodia nyimbo za injili ikiwa ni njia ya kuendeleza kutangaza injili ya Mungu kupitia uimbaji pamoja na kuwezesha kwaya kujitegemea kiuchumi.
Uzinduzi wa stulio hiyo ya NMC ulikwenda sambamba na kusimika wazee wa kanisa hilo wa usharika wa Nyakato, Igoma na Igombe uliofanyika katika Kanisa la Moravian Nyakato Wilayani Ilemela Mkoani Mwanza.
Akizungumza katika hafla hiyo, Askofu wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Magharibi, Ezekiel Yona amewapongeza Ushirika wa Nyakato kwa kuzindua studio hiyo kwani itasaidia sana kupeleka injili ya Bwana kwa watu kupitia rasilimali
Mbali na pongezi hizo, pia amewataka Wazee wa kanisa la Moravian Tanzania kutoka usharika mbalimbali jijini hapa kushirikiana na wachungaji na wainjilisti ili kuweza kutangaza injili na kudumisha amani kwa watu na Taifa kwa ujumla.
Askofu Yona, amesema ili kuendeleza kazi ya Mungu, kulinda amani na kuleta maendeleo ya Taifa, wazee hao wahakikishe wanashirikiana na wachungaji na wainjilisti pamoja na kuwa washauru wazuri kwa viongozi wao na siyo kuwasemea pembeni pale wanapo kosea.
Mchungaji wa kanisa la Moravian usharika wa Nyakato, Mchungaji Stephen Mhenga amesema, mradi huo wa ujenzi wa studio uliogharimu zaidi ya Sh. milioni 55 mpaka ulipofikia ulikua unahitajika fedha nyingi na walianza kujipanga kwa sababu waliona ikikamilika itasaidia kuondoa utegemezi wa wanakwaya kwa kanisa kupitia waumini.
“Kusudi letu katika studio hii ni mambo mawili la kwanza ni kutangaza injili kwa njia ya uimbaji kwani tunategemea kwaya nyingi zitatoka maeneo mbalimbali kutoka mikoa yote ya nchini Tanzania, mpaka sasa tuna oda ya kwaya sita kutoka mikoa ya Tabora, Shinyanga, Musoma na jambo hili ndio lililotusukuma kufanya kasi ya kutafuta fedha za kukamilika studio hii,” amesema Mchungaji Mhenga na kuongeza kuwa.
“Jambo hili limekuwa kusudi jema kwa watakao rekodi kupitia studio hiyo nyimbo zao watakazoimba watakuwa wametusaudia kutangaza injili huku kusudi la pili ikiwa ni uchumi tumeona sana kwaya yetu inategemea kanisa hivyo tukaona wakiwa na mradi huu utawasaidia kukusanya fedha ambazo zitawasaidia katika mambo mengine na kuboresha uimbaji wao,”.
Baada ya kufanikisha jambo hilo, wanataka kila kitu kifanyike kwenye studio hiyo ambapo watakuwa na upande wa kurekodia audio na video kwani malengo yao ni kuwa na miradi mingine itakayosaidia kuimarisha kanisa na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kwaya ya Nyakato Moravian, Ambilike Kyamba, amesema kwaya hiyo imefanya uzinduzi wa studio yake ambao wanategemea mambo mengi pamoja na kuwa chanzo cha kuinua uchumi wa kwaya na kanisa kwa ujumla kwani wameona vijana wengi wakipotea kutokana na hali duni ya uchumi hivyo wataajiriwa ili kuwaepusha kujiingiza kwenye vitendo viovu, kuwa tegemezi na kuinua pato la Taifa.
Mwalimu wa kwaya hiyo, Obedi Malando amesema, studio hiyo imetengenezwa kwa ajili ya kuwaleta karibu watu na kwa manufaa ya wengi katika kueneza injili, pia itarekodi vikundi vyote na wale wanaoimba nyimbo za injili tu, pia ni fursa kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa kukuza na kuibua vipaji mbalimbali vya kwaya na binafsi.
More Stories
15 wajinoa Juventus,akiwemo mtoto wa Mwenyekiti wa CCM Mbeya
Startimes yazindua makala ya China, Africa
Za Kwetu Fashion Show, yawapaisha wanamitindo nchini