Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Dar
MFANYABIASHARA maarufu nchini, Mohamed Dewji ‘MO Dewji’ anayemiliki kampuni ya Mohamed Enterprisses (MeTL) amesema katika kipindi cha miaka minne ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan, ataongeza ajira kutoka 31,000 za sasa hadi 100,000.
Ahadi hiyo ameitoa jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na baadhi ya wanafunzi wa elimu ya juu wanaofadhiliwa na Taasisi yake ya Mo Dewji Faoundation.
Amesema Rais Samia amerejesha uhusiano mzuri na mataifa mbalimbali na wawekezaji, jambo litakalosaidia kukua kwa uchumi wa Taifa, mtu mmoja mmoja na kuongeza ajira.
“Kuna mwelekeo mzuri chini ya Rais Samia, ninawaomba wafanyabiashara wenzangu tumuunge mkono Rais wetu kwa kuwa anataka tupige hatua kiuchumi na kukuza uchumi,” amesema.
Alisema Rais Samia anafanya vizuri katika kuwavutia wawekezaji wa nje na kuwalinda, hivyo baada ya miaka michache uchumi wa Tanzania utaimarika zaidi.
Kuhusu ufadhiili wa Mo Dewji Foundation kwa wanafunzi hao 100, amesema ulianza mwaka 2015 na kadri siku zinavyonde ndivyo anavyotarajia kuongeza zaidi idadi ya wanafunzi hadi 1,000, huku akilenga wafikie 10,000 katika miaka mitano ijayo.
“Mimi nawaomba mkishafanikiwa mkumbuke kuwasaidia na wengine kwa kuwa mimi sitaki mnirejeshee hata senti moja, lengo langu ni kuhakikisha tunapiga hatua na kuondokana na umasikini,” amesema.
Amesema kuwa tangu Mo Dewji Faondation ilipoanza zaidi ya sh. bilioni bilioni zimetumika katika mradi huo wa kuwafadhii wanafunzi vyuoni ili waweze kufikia ndoto zao.
“Uhitaji ni mkubwa, lakini tunaangalia zaidi wale wanaotoka katika mazingira magumu bila upendeleo wowote, tunazingatia usawa jinsia hata na dini,” amesema MO Dewji.
Katika mkutano wake na wanafunzi hao, MO Dewji alikumbushia tukio la kutekwa kwake lililotokea Oktoba 11, mwaka juzi katika Hoteli ya Colosseum jijini Dar es Salaam nchini alikokwenda kufanya mazoezi na aliachiwa Oktoba 20 katika viwanja vya Gymkhana baada ya kutelekezwa na watekaji.
Amesema alipotekwa siku tisa alijua atakufa, lakini Watanzania kwa umoja wao waliweza kumuombea na Mungu akasikia.
“Lazima nianze kumshukuru Mungu, lakini pia nina deni kubwa na nchi hii. Najua mnajua mimi nilitekwa siku tisa, nilikuwa najua nakufa, lakini Watanzania wameniombea na Mungu akawasikia, nina deni kwa Watanzania ndiyo maana sitaacha kujitolea kila nilichonacho kwa ajili yao.
Mmoja wa wanufaika hao, Miriam Ibrahim aliishukuru Taasisi hiyo kwani imewasaidia katika kuweza kufikia ndoto zao.
“Tumekuwa tukipata fursa mbalimbali kupitia taasisi hii ikiwemo wengine kupata kazi katika kampuni ya MELT. Natoa wito kwa taasisi zingine kuiga mfano huu,” amesema Miriam.
Naye Baraka Edward ambaye ni mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema: “Tukisema tukulipe kwa kile ambacho umekifanya hatuwezi, hata tukisema tuje kufanya kazi bure katika kampuni yako haiwezi kulipa jinsi ulivyotusaidia. Mungu akubariki sana MO, asante,” amesema.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi