Na George Mwigulu,Timesmajiraonline, Nsimbo.
MFUMO wa kielektroniki wa manunuzi wa Umma (NeST) umetajwa kuongeza uwazi, wajibikaji, ufanisi, usalama, kupunguza rushwa miongoni mwa watendaji serikalini pamoja na kuokoa fedha ambazo zinaweza kutumika kwenye miradi mingine ya maendeleo.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024,Godfrey Mnzava amebainisha hayo Septemba 11, 2024 katika kijiji cha Ibindi Halmashauri ya Nsimbo Mkoa wa Katavi wakati akifungua mradi wa ujenzi wa daraja la upinde wa mawe.
Mnvaza amesema kuwa hapo awali kulishuhudiwa malalamiko na manug’niko ya muda mrefu kuwapo kwa baadhi ya wakandarasi wakiamini kwa hisia kuwepo kwa upendeleo wa wakandarasi kupewa zabuni za ujenzi wa miradi mbalimbali hapa nchini.
“Mfahamu kuwa kupitia mfumo wa NeST malalamiko hayo hayapo lakini pia itaongeza uwazi na uwajibikaji mzuri na kuongeza udhibiti wa namna bora ya kuwapata wakandarasi hao kwani kila mmoja ataingia kwenye mfumo na kuona moja kwa moja”amesema Mnzava.
Ameongeza“Viongozi nao watakuwa na uwezo wa kuona namna mchakato ulivyofanyika kupitia mfumo wenyewe na hayo ndio maelekezo ya serikali kwenye utekelezaji wa miradi yote kwa fedha zinazotoka serikali kuu au kwa mapato ya ndani na wadau na wahisani wengine”amesema.
Kutokana na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) kuzingatia matumizi ya mfumo huo kwenye ujenzi wa mradi wa daraja la mawe amewapongeza huku akizitaka taasisi na mashirika yote ya serikali kuzingatia maagizo ya serikali.
“Manunuzi yote, iwe kumpata mkandarasi au kama ni kupata huduma na kama ni vifaa vyote ni kwenye mfumo na mambo ya kutangaza matangazo kwenye mbao za matangazo yamekwisha kupitwa muda mrefu” Amesisitiza Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Mfumo wa NeST ulitambulishwa rasmi Juni 23,2023 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA),Dkt.Leonada Mwagike kwa ajili ya kudhibiti ununuzi wa umma unaozingatia uwazi.
Mwenyekiti huyo wa Bodi hiyo alinukuliwa na vyombo vya habari akisema mahitaji mapya ya teknolojia pamoja na maelekezo ya serikali ya kuimarisha eneo la ununuzi ambapo PPRA ilianza zoezi la kusanifu mfumo huo hali inayosaidia misingi mikuu ya kimataifa ya ununuzi kuzingatiwa.
Dkt.Mwagike alinukuliwa akisema “ Mfumo huo wa NeST utakuwa mbadala wa mfumo unaotumika wa TANePS. Huo mpya unatatua changamoto za kiufundi na hivyo kukidhi mahitaji ya serikali katika sekta ya ununuzi”.
Afisa wa TARURA Wilaya ya Mpanda, Mhandisi Simon Munge akisoma taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa daraja Upinde la mawe Ibindi amesema kuwa ujenzi huo uliibuliwa na kuanza kujengwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 ambapo jumla ya fedha Mil 286.3 zimetumika.
Amesema daraja hilo kwa sasa umerahisisha usafiri kwa wananchi ambao wanaingia na kutoka katika kijiji cha Ibindi na viunga vyake kwa majira yote ya kila mwaka.
Masaja Anthony Mkazi wa kijiji hicho amesema kutokana na idadi kubwa ya wananchi ni wakulima hivyo imewarahisishia kusafirisha mazao yao kutoka shambani hadi nyumbani au sokoni kwa ajili ya kuuza.
Amesema daraja hilo ni msaada mkubwa kwa vijiji cha Ibindi, Makambu, Itenka A, Itenka B na Tulieni ambapo hapo itawasaidia pia kupata mahitaji mbalimbali ya kijamii kutoka maeneo mengine.
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais