Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline, Korogwe
MBUNGE wa Jimbo la Korogwe Vijijini mkoani Tanga Timotheo Mnzava amesema ameanzisha mashindano ya mpira wa miguu kwa kata zote 29 za jimbo hilo ili kuibua vipaji kwa vijana ili waweze kuchezea timu kubwa na kupata ajira.
Mnzava amesema kwa sasa mchezo wa soka ni ajira kubwa ndani na nje ya nchi hivyo ili kuweza kuwaibua vijana hao na kuweza kwenda kuchezea timu za Simba, Yanga, Azam ama Coastal Union ni lazima uandae michuano kama hiyo.
Ameyasema hayo Septemba 29, 2024 mara baada ya fainali ya Mnzava Cup kati ya timu ya Kata ya Lutindi na Kata ya Kwashemshi iliyofanyika Shule ya Msingi Lewa na Lutindi walitwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa ushindi wa 1-0 na kuondoka na kombe,sh.750,000, jezi jozi moja, mipira miwili na wachezaji kuvikwa medali za dhahabu.
“Michezo ni miongoni mwa Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (2020-2025). Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake, wamekuwa wakituelekeza, wakituusia na kutushauri kuhakikisha vijana wanashiriki shughuli za michezo. Moja ya faida ya michezo ni kujenga mahusiano, kupata burdani na kwenye michezo pia kunavumbuliwa vipaji na kwenye michezo hii kuna watu walikuwa wanafuatilia na wameona vipaji vingi kutoka kwa vijana.
“Nataka niwahakikishie, wale vijana wote waliofanya vizuri ambao wamekuwa na vitu vya ziada ndani mwao, hawataishia kwenye michuano hii,tutawatafutia sehemu ya kwenda ili kufanya majaribio na tuone namna ya kusogea kwa kupata timu nyingine, wale ambao Mwenyenzi Mungu atawabariki waweze kupata ajira kupitia vipaji vyao ambavyo Mungu amewapa” alisema Mnzava.
Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Mkoa Tanga Mussa Shekimweri amesema pamoja na kuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Korogwe miaka 10 na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga miaka 10, hajaona Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini amefanya jambo kubwa kama hilo na kupongeza jitihada hizo za kuibua vijana ziendelee.
Mgeni rasmi kwenye ufungaji wa fainali hiyo Tarafa ya Bungu, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Korogwe Vijijini Ally Waziri, alisema pamoja na jitihada kubwa za shughuli za maendeleo zinazofanywa na Mnzava, bado anafanya mambo makubwa kwenye michezo, jambo hilo litasaidia kuibua vipaji vya vijana, kuwaleta watu karibu na kuimarisha michezo kwenye Jimbo la Korogwe Vijijini.
Katibu wa CCM Wilaya ya Korogwe Vijijini Safina Nchimbi amesema pamoja na michezo, vijana wanatakiwa kuipenda nchi yao, hivyo wanatakiwa kushiriki kupata viongozi wa vijiji, vitongoji na mitaa kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, mwaka huu.
Mratibu wa Michuano hiyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Dindira Selemani Mwongozo, alisema michuano hiyo ilianza kwenye ngazi ya vijiji, ambapo Mnzava alitoa jezi jozi mbili na mipira mitatu ili vishindaniwe ndani ya kata, na baada ya kupatikana timu ya kata, ndipo ikaanza michuano ya kata kwa kata ngazi ya tarafa na baada ya kupata mabingwa wa tarafa, kutakuwa na michuano ya tarafa kwa tarafa ili kupata Bingwa wa Jimbo, Mnzava Cup.
Mwongozo alisema katika michuano hiyo ngazi ya tarafa, mshindi wa pili hadi wa nne nao walipata fedha, medali, jezi na mipira.
More Stories
15 wajinoa Juventus,akiwemo mtoto wa Mwenyekiti wa CCM Mbeya
Za Kwetu Fashion Show, yawapaisha wanamitindo nchini
TCAA yaadhimisha siku ya usafiri wa anga Duniani kwa kushiriki mbio za Marathon UDSM