Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti amekabidhi madume bora 20 ya ng’ombe wa nyama kwa vikundi vya wafugaji wa kijiji cha Nyichoka Wilayani Serengeti na madume Bora 20 kwa vikundi vya wafugaji wa kijiji cha Mariwanda Wilayani Bunda, ili iwasaidie kuzalisha kizazi chenye uwezo wa kutoa nyama nyingi zaidi ya wale wa asili waliopo hapa nchini.
Akikabidhi, madume hayo Bora ya Ng’ombe kwa vikundi vya wafugaji katika hafla fupi zilizofanyika Septemba 27, 2024 Wilayani Serengeti na Bunda mkoani Mara, Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mnyeti amesema kuanzia mwaka wa fedha 2022/2023 Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikitekeleza mpango wake wa kuleta mabadiliko katika Sekta ya Mifugo, ambapo mpango huo umegusa nyanja mbalimbali za uzalishaji wa mifugo ili kuhakikisha ukuaji wa uhakika wa uzalishaji wa mifugo na mazao yake ili kukidhi ongezeko la soko la ndani na nje ya nchi.
“mpango huu unahusisha kuboresha mbari za mifugo, upatikanaji wa maji na malisho kwa ajili ya mifugo na kuhakikisha afya ya mifugo kwa kuwapatia wafugaji dawa za kuogeshea na kampeni ya chanjo”, amesema Mhe. Mnyeti
Aidha, Mhe. Mnyeti amesema hatua zingine zinazochukuliwa ni pamoja na kuboresha huduma za ugani kwa kuwapatia maafisa ugani mafunzo rejea na vitendea kazi vikiwemo pikipiki kwa ajili ya usafiri wa kuwafikia wafugaji, kuongeza fedha kwa ajili ya utafiti pamoja na kujenga na kuboresha masoko ya mifugo.
Vilevile, Mhe. Mnyeti amesema asilimia 97 ya ng’ombe walioko hapa nchini ni wale wa asili, ila ng’ombe hawa wa madume Bora ni wavumilivu kwenye masuala ya magonjwa pamoja na uhaba wa malisho na maji, na uzalishaji wake wa nyama ni wa juu ukilinganisha na ng’ombe wengine wa asili, kwani wameboreshwa kwa kuingiza vinasaba vya mbegu yenye uzalishaji mkubwa kwa kuchanganya mbegu za ng’ombe wa asili na wale wenye uzalishaji wa juu kunazalisha ndama mwenye sifa zaidi ya wazazi wake kwani anakuwa na uzalishaji mkubwa kuliko yule wa asili na kwa upande mwingine anakuwa na uwezo wa kuvumilia mazingira magumu kuliko yule mwenye uzalishaji mkubwa asiye wa asili.
Mhe. Mnyeti ameongezea kwa kusema, Wizara imefanya hivyo kwa vikundi kadhaa vya wafugaji kwenye Halmashauri mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kutoa hamasa kwa wafugaji ili kubadilika na kufuga kibiashara kwa kuwa na ng’ombe wenye tija.
Kwa Upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Uzalishaji Mifugo, Bw. Simon Lyimo amesema Wizara ya Mifugo imejipanga vyema katika kutatua changamoto mbalimbali za wafugaji pamoja na mifugo.
“tumechukua hatua mbalimbali za kuiboresha mifugo ili wafugaji waweze kupata mifugo bora na kufuga kwa tija”, amesema Bw. Lyimo
Naye, Kiongozi wa wafugaji Kanda ya Nyanza ambayo inajumuisha Mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga, Bw. Kikuri Mnikokostantine ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Dkt. Samia Suluhu Hassani kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya Mhe. Abdallah Ulege (Mb), kwa kuwapatia madume Bora ya ng’ombe na kuomba kuongezewa tena kama ikimpendeza Mheshimiwa Rais na Waziri mwenye dhamana.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best