January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mnara wa mawasiliano kujengwa kijiji cha Msolokelo Morogoro



Na Mwandishi Wetu,WHMTH, Morogoro.

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Jerry William Silaa (Mb) ametoa maelekezo kwa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kushirikiana na watoa huduma kujenga mnara wa mawasiliano katika kijiji cha Msolokelo, mkoani Morogoro ili kutatua changamoto ya ukosefu wa huduma za mawasiliano ya simu na intaneti katika kijiji hicho.

Waziri Silaa ametoa maagizo hayo leo Disemba 3, 2024 wakati wa ziara yake mkoani humo ya kukagua hali ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo yenye changamoto sambamba na kukagua ujenzi wa minara inayojengwa mkoani katika mkoa huo ikiwa ni sehemu ya ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano inayoendelea kujengwa kote nchini.

Waziri Silaa amewahakikishia wananchi wa Msolokelo kufikishiwa huduma za mawasiliano katika kipindi kifupi kijacho kwa kuwa Serikali ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan iko makini kuhakikisha kuwa vijiji vyote nchini vinapata huduma za mawasiliano kabla ya mwaka 2025 kumalizika.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa minara ya mawasiliano katika mkoa wa Morogoro, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mhandisi Peter Mwasalyanda amesema kati ya minara 69 inayotarajiwa kujengwa katika mkoa huo, hadi sasa minara 19 imekamilika na imeanza kutoa huduma.

Ameongeza kuwa kati ya minara hiyo iliyoanza kutoa huduma imewezesha kijiji cha Pemba na baadhi ya maeneo ya kijiji cha Gonja vilivyopo katika kata ya Pemba, kupata huduma za mawasiliano kwa mara ya kwanza kupitia ujenzi wa minara hiyo.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Mwasalyanda amesema baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Morogoro ikiwa ni pamoja na Kijiji cha Msolokelo yana milima ambayo ndiyo imekuwa kikwazo kwa wananchi kupata mawasiliano ambapo kama kusingekuwa na milima kijiji hicho kingeweza kupata mawasiliano kutoka kwenye mnara wa kijiji cha Pemba.

Aidha, amesema kuwa Serikali itashirikiana na mtoa huduma ambaye ni Vodacom Tanzania kuhakikisha inajenga mnara mwingine katika Kijiji cha Msolokelo ili kutatua changamoto ya mawasiliano katika kijiji hicho.