March 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mmuya apongeza hatua ya ujenzi ofisi ya msajili wa vyama vya siasa

Na mwandishi wetu,timesmajira, Dodoma

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Bwa. Kaspar Mmuya amepongeza maendeleo ya ujenzi wa ofisi za msajili wa vyama vya siasa nchini zinazojengwa eneo la Kilimani Jijini Dodoma zitakazogharimu zaidi ya shilingi bilioni 20.

Naibu Katibu Mkuu huyo aliyasema hayo alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua ujenzi huo unaofanywa na kampuni kutoka China ya Group Six International Limited ukisimamiwa na mshauri kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi.

Amesema ujenzi unatarajiwa kukamilika baada ya miezi 12 akisisitiza kuongezwa kwa rasilimali watu, muda wa kazi pamoja na vifaa ili kufanya kazi ndani ya muda uliopangwa.

“Niwapongeze kwa kazi kubwa ambayo mnaifanya Ofisi ya Msajili wa vyama vya sisisa kwa usmamizi mkubwa mnaoufanya lakini endeleeni kuongeza umahiri na kuwasaidia wenzetu wa Group Six International wafanye kwa matokeo zaidi,” amesema Naibu Katibu Mkuu huyo.

Pia amemuagiza mshauri wa ujenzi kufika mara kwa mara katika eneo la mradi na kufanya kazi kwa kushirikiana na watendaji wengine kufahamu hali ya ujenzi na kutatua changamoto pindi zinapojitokeza kuhakikisha jengo linajengwa katika hali ya uimara, ubora na usalama.

“Nimshauri mtaalamu wetu awe anatembelea mara kwa mara jengo hili kujionea maendeleo ya kazi kama kuna shida yoyote inatatuliwa kwa wakati na kufanya marekebisho yanayaotakiwa,”amesisitiza .

Aidha amehimiza kuongeza ubunifu wa utendaji kazi kwa kugawa maeneo na muda wa kukamilika kwa kazi kwani itasaidia kuhamasisha kazi kufanyika kwa mwamko na ubora zaidi kama njia ya kuendana na muda wa mkataba unavyotaka.

“Waongeze mtindo wa kufanya kazi kwa kupewa kipande cha kazi kwa muda inasaidia utendaji wa kazi na waangalie ubora usiathiriwe kwa sababu mtu anapopewa eneo lake na muda wa kikomo inamfanya ajitume kwa kasi kubwa,” amesema Mmuya.