March 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mmoja afariki,33 wajeruhiwa ajali ya tingatinga na coaster

Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online,Songwe

Mtu mmoja amefariki dunia na wengine 33 wamejeruhiwa baada ya gari la abiria aina ya Toyota Coaster lenye namba za usajili T 691 DSM kugongana na Tingatinga (maarufu kama ‘Kijiko’),lisilokuwa na namba za usajili katika eneo la Nandanga, Halmashauri ya Mji Tunduma, Wilaya ya Momba, barabara kuu ya Ileje Mpemba.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga, amesema ajali hiyo imetokea Machi 10, 2025, majira ya saa 6:00 mchana, baada ya dereva wa Tingatinga hilo kuendesha kwa kuyumba barabarani,hali iliyosababisha kugongana na gari hilo la abiria, mali ya Bobu Mwampashi, ambalo lilikuwa likiendeshwa na Juma Mwafyabo (47).

Kwa mujibu wa Senga, amesema Sara Mzopola (37), aliyefariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mji wa Tunduma, iliyopo eneo la Mpemba.

“Tunaendelea kumsaka dereva wa Tingatinga ambaye alikimbia baada ya kusababisha ajali hii,ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake,”amesema Senga.

Amesema,awali majeruhi wote 33 wa ajali hiyo walikimbizwa katika Hospitali ya Halmashauru ya Mji Tunduma, ambapo 11 walilazimika kupewa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kutokana na hali zao kuwa mbaya, huku majeruhi 14 wakiruhusiwa kurejea nyumbani baada ya matibabu.

Ameongeza kuwa, majeruhi wengine nane wanaendelea kupata matibabu katika Hospitali hiyo ya Halmasgaurina kwamba hali zao zinaendelea vizuri.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Dkt. Sebastia Siwale, amekiri hospitali hiyo kupokea majeruhi wote 33 na kwamba hivi sasa inaendelea kuwahudumia majeruhi nane tu.