April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mlundikano wa madeni Halmashauri yamuumiza kichwa DED

Na Israel Mwaisaka,Sumbawangao

Uongozi wa halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, unaumiza kichwa kutatua changamoto ya mlundikano wa madeni yanayoikabili halmashauri hiyo.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga, Catherine Mashalla alisema hayo jana katika hafla fupi ya kukabidhi gari aina ya Coaster yenye thamani ya Sh milioni 65.8 kwa viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Manispaa ya Sumbawanga, hafla iliyofanyika katika ofisi za CWT mkoani Rukwa.

Alisema kwamba madeni halali yaliyohakikiwa ambayo halmashauri hiyo inadaiwa na watumishi wake na wazabuni ni zaidi ya Sh 2.9 bilioni fedha ambazo wanapambana kuzilipa kadri wanavyokusanya kutoka katika vyanzo mbalimbali vya mapato yao.

“Watumishi kwa ujumla wakiwemo walimu wanadai Sh 1.5 bilioni 1.5 fedha zilizotokana na likizo, uhamisho madeni ya wastaafu……huku Sh 1.4 bilioni zikiwa ni madeni ya wazabuni” alisisitiza

Alisema wameiomba serikali kuu iwasaidie kulipa baadhi ya madeni kwa kuwa kwa halmashauri pekee ni mzigo kubwa, ukilinganisha na makusanyo yao ambapo kwa mwaka wanakusanya Sh 2.7 bilioni.

Ambapo asilimia 40 ya mapato hayo upelekwa kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kiasi kinachobaki ni kwa ajili ya matumizi ya ofisi katika ngazi ya juu hadi kata.

Awali, Mwenyekiti wa CWT Manispaa ya Sumbawanga, Mwl. Huruma Kilingo alisema Walimu peke yao wanaidai halmashauri hiyo Sh 197 milioni zikiwa ni fedha za likizo, matibabu, uhamisho na kwenda masomoni.

Alisema gari hilo litawasaidia walimu katika utatuzi wa changamoto mbalimbali ikiwemo nyakati wanapopatwa na misiba ambapo kuna nyakati mwajiri anashindwa kutoa gari kwa walimu akifiwa na ndugu hivyo itakuwa fursa kwao kutumia chombo hicho cha usafiri.