January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mloganzila yawapongeza wafanyakazi wanawake MSD

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Naibu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi amewashukuru watumishi wanawake wa Bohari ya Dawa (MSD) kwa msaada wa kulipia sehemu ya gharama za matibabu kwa watoto wenye matatizo ya vichwa vikubwa na mgongo wazi, wanaohitaji kufanyiwa upasuaji.

Dkt. Magandi amesema gharama za matibabu hususani kwa watoto wenye changamoto za matibabu ya mgongo wazi na vichwa vikubwa ni kubwa sana, hivyo watu wengi hushindwa kuzimudu kama hawana bima ya afya na hivyo kuwaomba wadau kuendelea kujitokeza kuwasaidia, ili kurudisha tabasamu la watoto hao.

“Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Prof. Mohamed Janabi napenda niwashukuru na kuwapongeza kwa kuona umuhimu katika kuelekea Siku ya Wanawake Duniani, mkaona mje Mloganzila kwa kutumia sehemu ya mapato yenu binasi kutoa sadaka kwa kuwashika mkono wanawake wenzenu ambao watoto wao wana mahitaji na kwa uwezo wao hawawezi kumudu gharama za matibabu” ameongeza Dkt. Magandi

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wanawake MSD, TUGHE Rehema Mosha amesema wanawake wa MSD wameamua kuadhimisha siku ya wanawake mwaka huu kwa kulipia sehemu ya matibabu ya watoto wenye changamoto ya mgongo wazi na vichwa vikubwa kutoka kwenye mifuko yao.

Aidha Rehema ameongeza kuwa pamoja na kulipia sehemu ya gharama za matibabu pia wametoa misaada midogo midogo ikiwemo dawa za meno, pampasi, sabuni na wipers ambazo zitawasaidia katika usafi wa watoto hao pindi wawapo wodini.